TAASISI ya
Twaweza imetoa matokeo ya utafiti wake, ambapo imebainika kuwa asilimia 79 ya
Watanzania wamepinga uamuzi wa Serikali wa kusitisha matangazo ya moja kwa moja
(Live ) ya Bunge.
Katika maoni yao, wananchi hao
wamedai kuwa ni haki yao ya msingi kufahamu kinachoendelea katika vikao
mbalimbali vya Bunge.
Utafiti wa taasisi hiyo
umefanywa katika maeneo tofauti ya Tanzania Bara kupitia mpango wake wa Sauti
za Wananchi.
Akitoa taarifa ya matokeo ya
utafiti huo jana jijini Dar e Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan
Eyakuze, alisema suala hilo limeonekana kutokuungwa mkono na wananchi wengi.
“Asilimia kubwa ya Watanzania
wanapinga uamuzi wa Serikali wa kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge.
Suala hili limeonekana kugusa hisia za watu wengi na maamuzi haya ya Serikali
yakionekana kutoungwa mkono.
“Katika utafiti huu wananchi
nane kati ya 10 wanapinga uamuzi wa hali inayodhihirisha kutoungwa mkono kwa
hatua hiyo,” alisema Eiyakuze.
Akizungumzia sababu walizozitoa
wananchi wanaotaka matangazo ya Bunge yarushwe moja kwa moja, Eiyakuze alisema
asilimia 46 walisema yanawafanya waweze kufuatilia utendaji wa wabunge
waliowachagua kwa kuwa huko ndio walikowatuma.
“Asilimia 44 wanasema ni muhimu
kwa sababu wananchi wanahaki ya kufahamu kinachoendelea bungeni, asilimia 29
wanasema matangazo ya moja kwa moja yalikuwa yanaaminika zaidi kwa watazamaji
na wasikilizaji kuona na kusikia wenyewe kile kinachoendelea tofauti na mfumo
wa kurekodi ambapo kuna baadhi ya mambo yanahaririwa.
“Asilimia 16 walidai kuwa
inafursa mwananchi kupata taarifa sahihi badala ya kuzisoma kwenye magazeti
huku asilimia 16 nyingine wakisema inawasaidia wanachi kufuatilia mijadala ya
Bunge kwa wakati”, alisema Eiyakuze.
Pamoja na hali hiyo mkurugenzi
huyo alisema katika utafiti huo asilimia 92 ya wananchi walisema kuna umuhimu
wa vipindi vya Bunge kurushwa moja kwa moja kupitia Luninga na redio bila
kujali gharama zilizoelezwa kuwa ndio chanzo cha kufikia uamuzi huo.
“Asilimia 88 walisema vipindi
vya Bunge virushwe ‘Live’ bila kujali gharama ukilinganisha na asilimia 12
ambao waliona ni muhimu suala la bajeti likazingatiwa,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema
asilimia 80 wanaona matangazo ya moja kwa moja kutoka bungeni ni muhimu kama
yalivyo na asilimia 20 wakisema fedha hizo zitumike kwenye huduma nyinge za
jamii.
Akizungumzia suala la vyombo
vya habari vya binafsi kuruhusiwa kurusha matangazo hayo, Eiyakuze alisema
wananchi wanaunga mkono vyombo hivyo kuruhusiwa iwapo Serikali imeshindwa
kumudu gharama.
Utafiti huo pia umeonesha
Watanzinia wanne kati ya kumi wamewahi kuangalia matangazo ya moja kwa moja
kupitia Luninga na sita kati ya kumi wamesikiliza kupitia redio.
Aidha utafiti huo umeonyesha
zaidi ya nusu ya wananchi walosema wameangalia au kusikiliza vipindi vya Bunge
wamefanya hivyo ndani ya miezi miwili iliyopita.
Hali ilivyokuwa
Januari mwaka huu, Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alitoa ufafanuzi bungeni
kuhusu hatua ya Serikali kusitisha matangazo hayo kupitia Shirika la Utangazaji
la Taifa (TBC).
Miongoni mwa sababu
alizozieleza ni pamoja na kuwepo kwa gharama kubwa ya Sh bilioni 4.2
zinazotumika katika uendeshaji wa matangazo hayo ya moja kwa moja kwa mwaka pia
watumishi wa serikali kushabikia Bunge badala ya kuendelea na kazi ofisini.
Hatua ya Serikali kusitisha
matangazo hayo iliibua mjadala mkubwa bungeni huku Mbunge wa Kigoma Mjini,
Zitto Kabwe, (ACT-Wazalendo) akilitaka Bunge kusitisha shughuli zake ili
kujadili taarifa hiyo ya Serikali.
Siku chache baadaye kilio hicho
cha ukosefu wa fedha za kuonesha matangazo hayo ya moja kwa moja ambacho
kimekuwa kikitolewa na serikali, sasa kilipata ufumbuzi.
Hatua hiyo iliyokana na uamuzi
wa Mfuko wa Vyombo vya Habari nchini (TMF), kujitokeza hadharani na kueleza
kwamba upo tayari kutoa fedha zinazohitajika ili kuhakikisha haki ya Mtanzania
kupata habari kupitia TBC haiingiliwi wala kubughudhiwa kwa hoja yoyote.
Endapo Serikali itakubali ombi
hilo, wananchi wataendelea kunufaika na vikao vya moja kwa moja vya Bunge
tofauti na pendekezo la serikali la kunakili baadhi ya sehemu na kisha
kuoneshwa usiku.
|