MAFUNDI FC KUTIMBA VIWANJANI ILI KUSHIRIKI LIGI YA MKOA.
MAFUNDI FC KUTIMBA VIWANJANI ILI KUSHIRIKI LIGI YA MKOA.
TIMU ya Mafundi FC ya Tarime imeanza mazoezi kujiandaa kushiriki kwenye ligi ya mkoa baada ya kukaa nje kwa msimu mmoja wa 2015/2016.
Msemaji wa timu hiyo, Hussein Abeid aliliambia jamboleo jana kuwa timu hiyo imekuwa nje ya gemu kwa msimu mmoja kwa madai kuwa uongozi wa mkoa kuwa na timu zao zilizoandaliwa kupanda daraja.
Timu hiyo yenye mashabiki wengi wilayani hapa, imekuwa ikifanya vizuri kwenye ligi mbalimbali ikiwa ni ya Ester Matiko, kembaki, Ndesi na RPC kwa kipindi kirefu, hivyo kitendo cha kukaa benchi kiliwafanya mashabiki wake kukosa uhondo, ambapo sasa wataipata.
Abeid alisema kuwa tayari kikosi kinapiga mazoezi katika uwanja wa Serengeti mjini hapa na wameanza kufanya usajiri mapema ili kuwapata vijana wenye uwezo watakaowafikisha kwenye malengo yao.
Aliongeza lengo la kurudi dimbani ni kutaka kufikia malengo yake ya kupanda Daraja la pili hadi kufikia ngazi ya ligi kuu.
"Uwezo tunao na tunaona msimu huu uchaguzi ukifanyika viongozi watakaoingia ni wale wenye maona na soka la Mkoa wa Mara, na kwa uwezo wetu tunaenda kupanda daraja kwani hatuna timu ya kutuwekea kauzibe" alisema Abeid.