Wananchi wataka shule kufunguliwa



Wakazi wa kijiji cha Tatwe, kata ya Goribe, Wilayani Rorya, mkoani Mara, wameitaka serikali kufungua shule ya msingi Nyanjogu kuwapunguzia adha watoto wa chekechea wanaosoma katika shule hiyo kisha kwenda kuandikishwa katika shule ya msingi Tatwe iliyoko umbali wa zaidi ya kilomita 10.
 Wakazi hao walisema kuwa watoto wao wanaotaka  kitongoji cha Nyanjogu hutembea mwendo mrefu kwenda kutafuta masomo katika shule ya msingi Tatwe na wengine wakiugua na kulala njiani  kutokana na umri wao.

Shule hiyo iliyojengwa kwa nguvu za wananchi miaka mitatu iliyopita, ina vyumba viwili vya madarasa  na ofisi ya walimu lakini  haijafunguliwa rasmi kutokana na kutotim iza matakwa ya uongozi wa halmashauri kwa kufikisha vyumba vinne vinavyotakiwa na kukamilisha ujenzi wa nyumba ya mwalimu ambayo iko kiwango cha kupauliwa.

 “Watoto wakiugua wanalala njiani kwa sababu ya mwendo mrefu wanaotembea na kwa kuwa wanachoka wanalala njiani, juzi nilimkuta mtoto ameugua na kulala njiani baada ya kuzidiwa na kutembea kwa mwendo mrefu kurudi nyumbani” alisema Jeshi Nyango mwenyekiti wa kijiji cha Tatwe.
Hata hivyo Diwani wa kata ya Goribe Lucas Ong’eto alisema kuwa kuchelewa kukamilika kwa shule hiyo kunatokana na viongozi wa kisiasa kuingilia utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kuusababisha kuwa mgumu kwa kuwagomesha wananchi kutokana na utofauti wa kiitikadi.

“Nilienda halmashauri kuomba waje kufungua shule ile nikaambiwa  kuongeza vyumba viwili vya madarasa, choo cha wanafunzi na kukamilisha nyumba ya mwalimu. Nilipoitisha wananchi kwenye mkutano wa kuchangia maendeleo hawakuonekana nikakaamwenyewe  tangu saa nne asubuhi hadi saa 10 jioni  nikarudi nyumbani bila mtu mmoja kuonekana” alisema Ong’eto.

Mbunge wa jimbo la Rorya lameck Airo aliliona suala hilo la watoto kuugua na kulala njiani kuwa ni zito akaitaka kamati ya shule kesho yake  juni 20 kufuata vifaa vya ujenzi ili kukamilisha sehemu iliyobaki wanafunzi wanapofungua shule july saba waanze masomo mara moja.

“Kwa kuwa mabati yanayohitajika ni 46 kwa ajili ya kupaua nyumba ya mwalimu kesho mje mkachukue ofisini kwangu, na mifuko 20 ya saruji ili kukazia sehemu iliyobaki. Na baada ya kukamilika diwani uende kwa mkurugenzi mtendaji kumtaka aruhusu shule hiyo ifunguliwe kuwanusuru watoto”alisema Airo.




Powered by Blogger.