Mwenyekiti wa kijiji atajwa kukumbatia wezi Rorya:
Mwenyekiti wa kijiji atajwa
kukumbatia wezi
Rorya:
Wanakijiji cha Kitembe kata ya
kitembe Wilayani Rorya wameonyesha kutokuwa na imani na mwenyekiti wa kijiji
hicho Andrew Odiwa wakimtuhumu kushirikiana na wezi katika kata ya Kitembe na
kuiletea sifa mbaya Wilaya.
Walisema kuwa Odiwa
yeye kama kiongozi waliyemwamini na kumchagua hashirikiani nao katika
shughuli za maendeleo kijijini badala yake diwani ndiye huzifanya huku vikao
vikiitishwa kwa ajili ya maendeleo yeye huitisha mgomo kwa baadhi ya wananchi
akidai anazungumzia mambo ya chama.
Walisema hali hiyo imewafanya
wamtilie shaka kuhusiana na nafasi aliyonayo kwao, kuwa haifai badala yake
aondolewe ili kupisha mtu mwingine aishike kwa muda wakati uchaguzi
ukisubiriwa kufanyika.
Katika mkutano wa kata ulioitishwa
na diwani wa kata ya Kitembe Thomas Patrick ukishirikisha viongozi wa
ofisi ya mkuu wa Wilaya, jeshi la Polisi mkoa wa Tarime Rorya kujadili Wizi na
wezi wa mifugo katani humo ukifanyika kijiji chaKitembe, mwenyekiti wa kijiji
hicho aliitisha kikao cha chama cha mapinduzi huku akipinga kufanyika kwa mkutano
huo kijijini hapo.
Wananchi hao walisema wako tayari
kukaa bila kuwa na kiongozi kwa kuwa miaka miwili iliyopita Odiwa alinusurika
panga za wananchi baada kutajwa kuhusika kwenye wizi wa ng’ombe waliokuwa
wakiibiwa kijijini hapo na kukimbilia kwa polisi kujinusuru.
“Kero yetu kubwa ni uongozi wa
kijiji haututendei haki, mwenyekiti ni mpinzani wa maendeleo yetu wanakijiji,
diwani anapoonyesha juhudi ya kuleta maendeleo, mwenyekiti anakuwa mpinzani wa
kuyapinga, hata leo hali halisi imeonekana kwa kutokuwepo kwenye mkutano
ulioshirikisha Mbunge kijijini kwake”alisema Lameck Nyang’era mkazi wa kitembe.
Hata hivyo mwenyekiti huyo
amedaiwa kwenda kutoa ushahidi kwa polisi pale wezi wanapokamatwa na kufikishwa
kituoni kuwa si wezi bali kilichofanyika ni fitina na wezi kuachiliwa kurudi
kuwatishia wanaotoa ushahidi.
“viongozi tuliowachagua
wanashirikiana na wahalifu kwa kupewa pesa ili wawatetee, mwenyekiti wa kijiji
amekuwa akitoa ushahidi wa uongo polisi wa kuwatetea majambazi kuwa sio”
alisema Charles Ongiro mkazi wa kitembe.
Diwani wa kata hiyo Thomas Patrick
alito m wito kwa mkuu wa Wilaya na jeshi la polisi kusikia kilio cha wananchi
wa kata ya kitembe wanapolia kuwa wanashida ili wasaidiwe pale wanapowambia
kuwapo mwizi.
Patrick aliwatahadharisha wananchi
hao kuwa ikiwa hawataona umhimu wa kudhibiti wezi kwa kuwataja waziwazi itafika
wakati ambapo vijana wa kike na kiume wasipate pa kutembelea kutokana na sifa
zao kuwa mbaya kwa wizi na ushirikina ulioko katani hapo.
“Itafika wakati hata mabinti zetu
wataogopwa hata kuposwa kutokana na uchawi ulioko katani humo, kata yetu
inasifika kwa wizi na uchawi, hii ni aibu kwetu wanakitembe,wachawi ninaowaomba
muone aibu muachane na tabia hii chafu”alisema Patrick.
Diwani huyo aliongeza kuwa suala la Wizi
wa Mifugo litamalizwa na wanakijiji wa kitembe endapo wataunganisha nguvu
ya pamoja na kuonesha ushirikiano wa pamoja .
Hata hivyo diwani huyo alizidi kukemea
suala la Ushirikina ambalo linazidi kuendelea kijijini hapo kwa hivi karibuni
kijana alipotea takribani siku tatu na kurejea siku ya tatu akiwa bubu
‘Jamani ondokana na Suala la Uchawi vijana
ni wenu kwanini munawapoteza kwa njia zisizoeleweka tutafikia hatua tuwatengee
wachawi wote’ alisema diwani.