SIMAMIENI MAENDELEO NA HAKI ZA WATOTO.
MEATU:
Wananchi na wakazi wa
Mkoa wa Simiyu wametakiwa kusimamia, kuimarisha na kuendeleza haki za
watoto ili kila mtoto aliyefikisha umri wa kuanza shule anaandikishwa ili
kwenda sambamba na malengo ya millennia.
Akiongea katika maadhimisho
ya siku ya mtoto Duniani kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Simiyu Paschal Mabiti,
mkuu wa Wilaya ya Bariadi Erasto Sima alisema viongozi simamieni haki za
watoto, ambapo maadhimisho hayo Mkoa wa Simiyu yalifanyika katika
Uwanja wa stendi ya mabasi Wilaya ya Meatu.
Sima alisema kuwa haki ya
mtoto ni mahitaji yote muhimu yaliyo ya lazima na anayopaswa kupatiwa
mtoto ili kumjengea msingi mzuri na bora wa maisha yake ya baadae atakapokuwa
mtu mzima ili awe mwenye kulifaa taifa na jamii kwa ujumla.
Alisema kuwa lengo la taifa
ni kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bora na kwamba jamii kwa
kushirikiana na serikali iweze kuimalisha ujenzi wa madarasa zaidi ili kuruhusu
watoto wote wenye umri wa kwenda shule kupata elimu bora.
Sima alisema kuwa pamoja na
kuweka msisitizo wa upatikanaji wa haki za watoto mkoani hapa zipo changamoto
nyingi ambazo zinachangia kutokuelewa kikamilifu haki za watoto ambao
wanaonekana kutengwa na jamii.
Alizitaja changamoto hizo
ni pamoja na ukatili wa wazazi/walezi kwa watoto ikiwa ni kuwapiga au
kuwapa adhabu kubwa zisizostahili na umri wao, kuwepo kwa ubaguzi unaotolewa
na wazazi katika kumpatia mtoto haki yake ya elimu.
Changamoto zingine ni mtoto
kutumikishwa kazi nyingi na ngumu kulingana na uwezo wake kwa kuchunga mifugo,
kulima, kufanya biashara ndogondogo, watoto wengine kutunza familia, kufanya
kazi za nyumbani hasa kwa watoto wa kike.
“tusimamie maendeleo na
makuzi ya watoto haipendezi kuona jamii kubwa inayotegemewa na taifa ikiwa
imepoteza mwelekeo wa maadili mema wakati sisi wazazi bado tungali hai”Alisema
Sima
Kwa upande wake Afisa
maendeleo ya wilaya ya Meatu Egiekiel Mkuki alisema kuwa licha ya kuwepo na
changamoto hizo wanayo mikakati mbalimbali ya kuweza kuwasaidia watoto kupata
elimu bora na kuweza kukua katika maadili ya kitanzania.
Mkuki alisema serikali
inahakikisha inaunda mabaraza ya watoto pamoja na kamati za halmashauri ambazo
zitakuwa zinasimamia matatizo ya watoto katika wilaya na kutatua matatizo
ya watoto ambayo yatajitokeza ili kuweka mazingira mazuri ya watoto kuweza
kusoma na kupata elimu bora.
MWISHO
|