Makonda Kula Sahani Moja na Vigogo Waliogoma Kupima DNA....."Tusijaribiane, Mimi sio Mtoto Wenu"
Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kuwa atahakikisha
anawashughulikia kwa mujibu wa sheria na mamlaka aliyonayo, wanaume
wanaokataa kuitikia wito wa kufika katika ofisi zake kujibu tuhuma za
kutelekeza watoto na kupima vina saba (DNA).
Akizungumza kupitia TBC1, Makonda amesema kuwa wanaokataa wito huo wakidhani kuwa hadhi yao ni muhimu zaidi wanapaswa kufikiria tena kwani bahati nzuri watu hao wanamfahamu hata kabla hajawa mkuu wa mkoa.
“Yoyote
anayekaidi wito wa Ustawi wa Jamii ambao wako chini yangu, achilia
mbali kwamba anakuwa amefanya kosa kwa mujibu wa sheria, kwa mamlaka tu
niliyonayo mimi nakutia ndani,” alisema.
“Yaani
na bahati mbaya niwaambie tu Watanzania, kwangu sheria ina nafasi kubwa
sana kuliko hadhi unayojitengenezea ambayo kimsingi huna kama umeamua
kutelekeza mtoto. Tusijaribiane,” aliongeza.
Mkuu
huyo wa mkoa alieleza kuwa anayetunisha misuli ya kutoitikia wito
anapaswa kufikiria kuwa kama anaweza kumuondoa mtu kwenye mkoa huo
anapoona anahatarisha usalama na kuvunja amani, itakuwaje kwa hilo la
mtu kumtelekeza mtoto.
Alisema
kuwa awali, wanasiasa waliokuwa wanajinasibu kuwa hawahusiki na
kinachoendelea na kwamba ni mpango wa kuchafuana kisiasa wameanza kuwa
wapole baada ya kuona mama na watoto waliowatelekeza wakijitokeza na
kuzungumza hadharani.
Akizungumzia
hatua anazoweza kuwachukulia watu hao, Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa
baada ya Ustawi wa Jamii na dawati la wanawake la Polisi kukamilisha
kazi ya kuwaita wanaolalamikiwa kukamilika, watampa ripoti ya
walioitikia wito na waliokataa pamoja na hatua walizofikia na ndipo
waliokaidi watajua wigo wa mamlaka yake.
“Nikiambiwa
haya mashauri yamebaki hayajashughulikiwa kwa sababu walioitwa wamegoma
kuja… sasa hapo ndipo utaelewa Makonda ni Mkuu wa Mkoa, mwenyekiti wa
kamati ya ulinzi na usalama au ni mtoto wako unayeweza kumuendesha kama
unavyoweza kuchezea sharubu za Simba aliyelala,” alisema.
Miongoni
mwa watu maarufu wanaotakiwa kufika katika ofisi za mkuu huyo wa mkoa
ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye analalamikiwa na
mwanamke mwenye umri wa miaka 31 kuwa ni mtoto wake aliyemtelekeza. Mama
mzazi wa mtoto huyo pia alifika katika ofisi hizo na kueleza kuwa
anachosema mwanaye ni kweli kwamba baba yake ni mzee Lowassa.
Mwingine
aliyeguswa na sakata hilo ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter
Msigwa ambaye naye amekataa kufika ofisi za mkuu wa mkoa na kumtaka
mwanamke anayedai kuwa alizaa naye na kumtekeleza afike katika ofisi za
bunge ataonana naye.
Msigwa alisema kuwa endapo itathibitika kuwa ni mwanaye yuko tayari kuacha ubunge.