Wadaiwa sugu Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) wapewa siku saba
Benki
ya Wanawake Tanzania (TWB) imetangaza kuzipiga mnada mali za wadaiwa
sugu 7,065 watakaoshindwa kulipa madeni yao ndani ya siku saba kuanzia
jana.
Mwenyekiti
wa bodi wa benki hiyo, Beng’i Issa alisema jana Machi 6 kwamba uamuzi
huo ni sehemu ya kukabiliana na ongezeko la mikopo chechefu au
isiyolipika iliayo.
“Mpaka sasa mikopo isiyolipika imefia Sh7.9 bilioni hivyo kuongeza ugumu kidogo katika kuhakikisha tunapata mtaji wa kutosha,” alisema Issa.
Ndani ya muda walioutoa, alisema wateja wanaodaiwa wanapaswa kulipa madeni yao ambayo ni ya muda mrefu.
“Wengi wameshapitiliza siku 90 za kutorejesha madeni yao kinyume na utaratibu na makubaliano na benki,” alisema
Kwa
watakaoshindwa kulipa fedha hizo ndani ya muda uliotolewa wa benki
kuchukua hatua za kisheria kabla ya kunadisha dhamana zao, amesema wenye
dhamira ya kulipa waende kwenye tawi lolote la benki hiyo wakiwa na
mpango mahususi wa jinsi watakavyofanikisha malipo yao.
Januari
4, wakati Benki Kuu Tanzania (BoT) inatangaza kufuta leseni za baadhi
ya benki nchini, TWB ilipewa agizo la kuongeza mtaji ndani ya miezi sita
ili kukidhi mahitaji ya ukwasi unaohitajika.
Kulingana
na masharti ya taasisi za fedha na benki za biashara nchini, kila moja
inatakiwa kuwa na mtaji na ukwasi wa kutosha kukidhi mahitaji ya kila
siku.
Wakati
TWB ikipewa onyo hilo, benki za Covenant, Efatha, Benki ya Wananchi
Njombe, Kagera Farmer’s Cooperative Bank na Benki ya Wananchi Meru
zilifutiwa leseni.
Mkurugenzi
mtendaji wa Benki ya Wanawake Tanzania, Japhet Justine amesema sheria
inawaruhusu kuuza mali au dhamana za wateja walizoweka endapo
watashindwa kurejesha mkopo kwa wakati waliokubaliana.
“Mbali
na kupiga mnada mali zao, taarifa zao tutazipeleka Benki Kuu ya
Tanzania wasiweze kupata mkopo katika benki nyingine yoyote nchini,”
alisema Justine.
Alisema
tangu kutolewa kwa taarifa ya awali kuwa benki ipo katika hali mbaya,
wamekusanya zaidi ya Sh2 bilioni kutoka kwa wadaiwa walionao, hatua
ambayo alisema ni nzuri.
Kwa
sasa, alisema wapo katika maongezi na wadau mbalimbali kuwawezesha
kupata mtaji waliowekewa na Benki Kuu na kwamba mwelekeo unaonekana kuwa
mzuri.
“Baada
ya benki yetu kupewa maagizo ya kuongeza mtaji na Benki Kuu tunapokea
wateja na wageni wengi wanaohitaji ufafanuzi kuhusu fedha zao lakini
wote wanaelewa,” aliongeza.