MEYA AKATAA GARI LA KUTEMBELEA ANUNUA GARI LA KUSOMBEA TAKA
Uamuzi wa Meya wa Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi Willy Mbogo
wa kukataa kununuliwa gari la kutembelea umewanufaisha wananchi
baada ya fedha zilizotengwa kiasi cha zaidi ya shilingi milioni
150 kwa ajiri ya kununua gari lake kutembelea na kuamua nunua gari
la kusombea takataka.
Awali Manispaa hiyo ilitenga kiasi cha Tshs 159,000,000/= kwa
ajiri ya gari la Meya ,lakini meya wa Manispaa hiyo Willy Mbogo
alikataa na kueleleza fedha hizo zielekezwe kwenye miradi ya
maendeleo kwa kununua gari la kusombea taka .
Gari hilo lori lenye namba za usajiri SM 12244 lenye uwezo
wa kubeba tani 16 lilikabidhiwa leo kwa uongozi wa Manispaa
hiyo katika ofisi za Manispaa hiyo zilizoko katika Mtaa wa
Ilembo ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpanda
Lilian Matinga.
Akisoma taarifa mbele ya mgeni rasmi kwenye makabidhiano hayo
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda Deodatus Kangu
alieleza kuwa Manispaa hiyo ilikuwa imetenga kiasi hicho cha
fedha kwa ajiri ya kununulia gari la kutembelea Meya wa Manispaa
hiyo ambaye hana gari la kutembelea kwa ajiri ya shughuli za
manispaa hiyo hata hivyo alikataa kununuliwa gari la badala
yake alielekeza fedha hizo zitumike kununua gari la kusombea
taka.
Kangu alieleza kuwa fedha hizo zilizokuwa zimetengwa kutokana na
makusanyo ya mapato ya ndani yaliyopatikana katika mwaka wa
fedha wa mwaka 2017 na 2018.
Alisema wakazi wa manispaa ya Mpanda huzalisha kiasi cha tani 70.5
za taka ngumu kwa siku sawa na tani 25,732.5 kwa mwaka
ambapo asilimia kubwa ya taka hizo ni taka toka majumbani na
maeneo ya biashara.
Kaimu Mkurugenzi Kangu alifafanua kuwa kutokana na upatikanaji
wa lori lenye uwezo wa kubeba tani 16 litasaidia kwa kiwango
kikubwa kuondoa tatizo la mrundikano wa taka ngumu zilizokuwa
zinabaki kwenye viziba au kwenye maeneo yaliyoandaliwa kwa muda
mrefu.
Alizitaja baadhi ya changamoto zilizopo katika katika
utekelezaji wa udhibiti wa taka ngumu katika Manispaa ya Mpanda
kuwa ni upungufu na uchakavu wa malori ya kuzoa taka na
kusafirisha taka ngumu .
Changamoto nyingine ni ongezeko la idadi ya wakazi inayopelekea
ongezeko la uzalishaji wa taka ngumu na ukosefu wa dampo la
kisasa kwa ajiri ya uchambuzi na uzikaji wa taka ngumu .
Mkuu wa wilaya ya Mpanda Lilian Matinga aliitaka Manispaa
hiyo kuhakikisha gari hilo linatumika kwa makusudio yake na
lisitumike kwa matumizi tofauti na yalivyokusudiwa .
Aliitaka manispaa hiyo kulitunza gari hilo la kulifanyia
matengenezo kila yatakapo hitajika na waakikishe gari hilo muda
wote linakuwa safi siyo kwa kuwa gari hilo ni la kusombea taka
basi waliache liwe chafu.
Pia aliishauri halmashauri hiyo isiishie kununua gari hilo tu
kwani mahitaji ya gari la kusombea taka bado yanahitajika kutokana
na jinsi manispaa hiyo inavyokuwa kwa kasi kubwa.
Haidari Sumry Diwani wa Kata ya Makanyagio alimpongeza Meya wa
Manispaa hiyo kwa uamuzi wake huo wa kizalendo aliuchukua kwa
manufaa ya wakazi wa manispaa na mkoa kwa ujumla.
Alisema jambo hilo la kubadili matumizi ya fedha zilizokuwa
zimetengwa kununulia gari lale ni jambo la kuigwa kwa
viongozi wengine.
Nae Meya wa Manispaa ya Mpanda Willy Mbogo alisema
uamuzi huo aliamua kuutoa sio kwa manufaa yake binafsi bali
alitanguliza maslahi ya wananchi kwanza na amewaomba wananchi
kuwaunga mkono pindi Manispaa hiyo wanapokuwa wanataka kuongeza
kipata cha Halmashauri hiyo.
Kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Mpanda Deodatus Kangu akisoma
taarifa fupi wakati wa mapokezi ya lori tani 16 kwa ajiri ya
uzoaji wa taka ngumu katika manispaa ya Mpanda.-Picha na Walter
Mguluchuma - Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Mpanda Lilian Matinga akimkabidhi meya wa manispaa
ya Mpanda Willy Mbogo funguo ya gari lori litakalotumika kwa
ajiri ya usombaji wa taka.
Meya wa manispaa ya Mpanda Willy Mbogo akimkabidhi funguo za gari
lori lenye namba SM 12244 Kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Mpanda
Deodadus Kangu.Picha na Walter Mguluchuma - Malunde1 blog