Video: Mbunge Nape Nnauye akosoa miradi ya serikali


Mbunge
wa Mtama kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amekosoa
utekelezaji wa miradi mikubwa unaofanywa na serikali ya awamu ya tano
chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli akidai kuwa inapelekea serikali
kukopa fedha nyingi kutoka kwa wadau wa maendeleo na hivyo deni la taifa
kuzidi kukua hali inayoweza kusababisha taifa kutokopesheka.


Nape
ameyasema hayo jana bungeni katika kikao cha pili cha mkutano wa 9 wa
bunge la 11 unaoendelea mjini Dodoma wakati akichangia Mapendekezo ya
Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/2019 na Mwongozo wa
Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2018/2019.


Nape
amesema kuwa hadi sasa kiwango cha serikali kukopa kimefikia asilimia
32 huku deni la taifa likiwa ni dola bilioni 26 na kusema kuwa miradi
mikubwa inayotekelezwa huenda ikapelekea serikali kukopa dola 21 bilioni
na hivyo kufanya deni la taifa kuwa dola 47 bilioni wakati ukomo wa
kukopa ni dola bilioni 45.

Miongoni
mwa miradi ambayo Nape ameikosoa ni pamoja na ujenzi wa reli ya kati
kwa kiwango cha kisasa (SGR), mradi wa kulifufua Shirika la Ndege la
Tanzania (ATCL) pamoja na mradi wa kufua umeme wa Stieglers Gorge katika
maporomoko ya Mto Rufiji mkoani Pwani.


Nape
ameeleza kuwa endapo serikali itaendelea kukopa ili kufadhili miradi
hiyo, italazimika kutumia fedha kutoka sekta nyingine kulipia madeni
hayo, jambo ambalo litakuwa likiumiza sekta hizo.


Aidha,
mbunge huyo alisema, kutokana na miradi inayotekelezwa sasa na serikali
ya awamu ya tano kuwa ya muda mrefu, serikali italazimika kuanza kulipa
madeni iliyokopa kutekeleza miradi hiyo kabla ya miradi yenyewe kuanza
kuwanufaisha wananchi, jambo ambalo litaifanya serikali kuchukua fedha
kidogo ambazo zinatokana na kodi za wananchi kulipa madeni.


Katika
hatua nyingine, Nape ameishauri serikali kuachana na utaratibu wa
kutaka kufanya kila kitu yenyewe, badala yake itengeneze mazingira
mazuri kwa ajili ya sekta binafsi kukua, ili kuepusha serikali kutumia
fedha zote inazokusanya katika miradi ya ujenzi wa miundombinu,
kuzalisha umeme, shughuli ambazo zingeweza kufanywa na sekta binafsi.


==>Msikilize Mbunge Nape Nnauye akizungumza hapa chini;
Powered by Blogger.