Rais Magufuli akutana na kufanya mazungumzo na watanzania waishio Uganda
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
amekutana na Watanzania waishio nchini Uganda katika Mji wa Masaka na
kuwahakikishia kuwa hatua zilizoanza kuchukuliwa na Serikali ya Awamu ya
Tano katika kuleta mabadiliko zimeanza kuzaa matunda.
Mhe.
Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli, Mawaziri na
viongozi wakuu wa taasisi za Serikali ametaja baadhi ya matokeo hayo
kuwa ni kusimamia vizuri uchumi unaokuwa kwa wastani wa asilimia 7,
kudhibiti mfumuko wa bei hadi asilimia 5.1, kuokoa Shilingi Bilioni 238
walizokuwa wanalipwa watumishi hewa kwa mwaka na kuondoa watumishi wenye
vyeti feki waliokuwa wakilipwa Shilingi Bilioni 142 kwa mwaka.
Matokeo
mengine ni kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka Shilingi Bilioni 850
hadi wastani wa Shilingi Trilioni 1.2 kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA),
kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge)
kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma umbali wa kilometa 726 ambapo Shilingi
Trilioni 7 zitatumika, kununua ndege 6 za Serikali kwa ajili ya kuinua
utalii na kuimarisha usafiri wa anga, kutoa elimu bila malipo kwa shule
za msingi na sekondari na kuboresha huduma za afya ikiwemo kuongeza
bajeti ya dawa kutoka Shilingi Bilioni 31 hadi 269.
Mhe.
Rais Magufuli pia amesema Serikali imechukua hatua madhubuti za
kuwavutia wawekezaji na sasa wengi wapo katika hatua mbalimbali za
uwekezaji ikiwemo ujenzi wa viwanda na ametoa wito kwa Watanzania hao
kuendelea kuwashawishi wawekezaji wengine kwenda kuwekeza nchini
Tanzania kwa kuwa fursa zipo nyingi.
Katika
mkutano huo Watanzania waishio Uganda wamemshukuru na kumpongeza Mhe.
Rais Magufuli kwa juhudi mbalimbali anazozifanya na wameomba Serikali
iwajengee mazingira bora pale wanapowapeleka wawekezaji nchini Tanzania.
Pamoja
na Mhe. Rais Magufuli kuahidi kufanyia kazi maoni ya Watanzania hao,
Mawaziri waliokuwa wakijibu hoja mbalimbali zilizotolewa wamewataka
kutosita kuwasiliana nao pale wanapokuwa na jambo linalohitaji majibu ya
Serikali.
Huu
ni mkutano wa kwanza wa Mhe. Rais Magufuli kukutana na Watanzania
waishio nje ya nchi (Diaspora), na Uganda kuna Watanzania 45,000 waishio
nchini hapa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Masaka, Uganda
10 Novemba, 2017