Rais Magufuli Aipongeza TANROADS Kuokoa Bilioni 4.5 za Mradi
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli jana
tarehe 07 Novemba, 2017 amefungua barabara ya lami ya Kyaka – Bugene
Mkoani Kagera yenye urefu wa kilometa 59.1 iliyogharimu Shilingi Bilioni
81.597 fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale
amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa barabara hiyo ni sehemu ya barabara
ya Kyaka – Bugene – Kasulo yenye urefu wa kilometa 183.1 ambayo
inaiunganisha Tanzania na nchi jirani za Rwanda na Burundi.
Kabla
ya kufungua barabara hiyo Mhe. Rais Magufuli akiwa na Mkewe Mama Janeth
Magufuli amesafiri kwa barabara hiyo kutoka Kyaka hadi Karagwe
zilipofanyika sherehe za ufunguzi na amempongeza mkandarasi, kampuni ya
CHICO ya China, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame
Mbarawa Mnyaa na timu ya wataalamu wa TANROADS kwa kuusimamia mradi huo
wao wenyewe kwa gharama ya shilingi Milioni 519.2 badala ya kuajiri
msimamizi ambaye angelipwa zaidi Shilingi Bilioni 4.5.
“Napenda
kuwapongeza sana TANROADS kwa kusimamia mradi huu nyinyi wenyewe, zaidi
ya Shilingi Bilioni 4 mlizookoa kwa kuwatumia wataalamu wetu kuusimamia
mradi huu ni fedha nyingi sana, nataka kitengo hiki cha usimamizi wa
miradi tukiimarishe, hivi sasa tunao wahandisi 15,000 wanaoweza kufanya
kazi hizi, tuwatumie” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe.
Rais Magufuli pia amezungumza na waandishi wa habari waliokuwa
wakirekodi na kurusha matangazo ya sherehe hizo ambapo amewashukuru kwa
kazi kubwa wanayoifanya na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea
kushirikiana nao, na ipo tayari kuwasaidia ikiwa ni pamoja na kuwezesha
mafunzo ya kuwaongezea ujuzi.
Sherehe
za ufunguzi wa barabara ya Kyaka – Bugene zimehudhuriwa na viongozi
mbalimbali wakiwemo Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe.
Charles Mwijage, Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, Wajumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakiongozwa na Prof. Norman
Sigalla King, Wabunge wa Mkoa wa Kagera na viongozi wa Dini na Siasa.
Akiwa
njiani kuelekea Karagwe Mhe. Rais Magufuli amesimamishwa na wananchi wa
Kyaka na kusikiliza kero zao ambapo amewaagiza viongozi wa Mkoa wa
Kagera kutowabughudhi wananchi wanaojihusisha na shughuli za kilimo, na
badala yake wawasaidie kuondoa migogoro ya ardhi, kusajili mifugo yao na
kuinua uzalishaji wa mazao ili Mkoa wa Kagera uwe na malighafi za
kutosha kuanzisha viwanda.
“Pale
Mtukula tumejenga kituo cha pamoja cha huduma mpakani (One Stop Border
Post) kati yetu na Uganda, lengo letu ni kurahisisha biashara kati ya
Tanzania na Uganda, kwa hiyo nataka kuona wananchi wa Kagera
mnachangamkia fursa hii, anzisheni viwanda kama vya nyama na mazao
mengine ya kilimo, fugeni mifugo kisasa ili mnufaike” amebainisha Mhe.
Rais Magufuli.
Akiwa
Bukoba Mjini kundi kubwa la wananchi wa mji huo limeusimamisha msafara
wake ambapo baada ya kupokea kero mbalimbali, Mhe. Rais Magufuli
ameahidi kutekeleza ahadi yake ya kutatua tatizo la uhaba wa maji katika
mji huo na ametoa wito kwa viongozi wa Manispaa ya Bukoba kuwasilisha
Serikalini andiko la kuomba kujengewa kituo cha mabasi kama wananchi
walivyomuomba.
“Ndugu
zangu mimi nipo pamoja na nyinyi, kero zenu nazijua na
tutazishughulikia, ninachowaomba punguzeni kubishana, mnapoteza muda
mwingi kubishana badala ya maendeleo, mnajichelewesha, Mji huu hautakiwi
uwe hivi ulivyo” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe.
Rais Magufuli kesho tarehe 08 Novemba, 2017 ataendelea na ziara yake
Mkoani Kagera ambapo atatembelea shamba la miwa na kiwanda cha sukari
cha Kagera kilichopo Misenyi na kujionea uwekezaji mkubwa na wa kisasa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Bukoba
