HOSPITALI YA MUHIMBILI KUOKOA MAMILIONI YA FEDHA TIBA YA INI
HOSPITALI
ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam, imeanza kutekeleza
mpango wa mwaka mmoja wa kuandaa watalamu kwa ajili huduma ya upasuaji
na upandikizaji ini.
Kwa mujibu wa taarifa ya MNH, hospitali hiyo kuu ya rufaa nchini, itakuwa ya kwanza kutoa huduma hiyo katika Afrika Mashariki.
MNH inaandaa wataalamu kwa ajili ya upasuaji ili kuondoa uvimbe ndani ya ini.
Wataalamu hao pia wataandikiza ini, na watatibu homa ya ini ili
kupunguza vifo vinavyosababishwa na magonjwa sanjari na kupunguza rufaa
zilizokuwa zinahitajika kwenda nje ya nchi.
Kwa sasa gharama ya tiba ya upasuaji na upandikizaji kwa mgonjwa wa ini
lililodhurika au kushindwa kufanya kazi, inafikia wastani wa Sh milioni
100 za Tanzania.
Wataalamu saba wa MNH wakiwemo madaktari na wauguzi, mwezi huu wanatarajiwa kwenda India kujifunza tiba ya ini.
Kwa mujibu wa daktari bingwa magonjwa ya tumbo na ini katika Idara ya
Tiba hospitalini hapo, Dk John Rwegasha, ndani ya mwaka kuanzia sasa
huduma ya uchunguzi wa mfumo wa ini na upasuaji mkubwa wa ini, itakuwa
imeanza hospitalini hapo.
Dk Rwegasha alisema hayo alipozungumza na HabariLeo kuhusu jitihada
wanazozifanya kupunguza vifo na rufaa za kwenda nje ya nchi kutibiwa
ini.
Kwa mujibu wa Dk Rwegasha, huduma hiyo itakapoanza MNH, hospitali
itakuwa ikiongoza kutoa huduma hiyo ya kibingwa miongoni mwa nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Alisema wamekuwa wakitoa mafunzo kwa madaktari wa ndani ya nchi na nchi
za EAC hasa Uganda kwa lengo la kutimiza azma, kuwawezesha watalaamu
kumudu huduma za tiba za awali kwenye eneo hilo.
Dk Rwegasha alisema kabla ya kuboreshwa kwa kitengo cha mfumo wa chakula
na ini mwaka 2014, walikuwa wakitibu wagonjwa wachache wenye matatizo
ya vidonda vya tumbo, lakini sasa wanatibu matatizo mengi ya aina
mbalimbali ya mfumo wa chakula na ini, yakiwemo ya saratani za koromeo
la chakula, uvimbe katika utumbo, kongosho, mfumo wa ini na nyongo kama
kutoa mawe na kuzibua uvimbe kwenye mifereji ya ini.
Kwa mujibu wa daktari huyo, pia wanazuia utapikaji damu unaotokana na
kusinyaa kwa ini, kunakochangia kupoteza damu nyingi na kupoteza maisha
kirahisi.
Hivi karibuni kitengo hicho kilianza kutibu wagonjwa wa homa ya ini na
kufikia sasa wastani wa wagonjwa 1,000 ndani ya mwaka mmoja wamefanyiwa
uchunguzi wa homa ya ini na tayari wagonjwa 100 wanapatiwa huduma bure
ya tiba homa ya ini kupitia ufadhili wa shirika la CDC.
IMEANDIKWA NA LUCY NGOWI - HABARILEO