CHADEMA YAMTAKIA KILA LA HERI KATAMBI....YAWASIHI CCM KUMTUMIA KADRI WATAKAVYOONA ANAFAA
Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji amesema chama hakina mgogoro na
aliyekuwa Mwenyekiti wa Bavicha, Patrobas Katambi ambaye ametangaza
kujiunga na CCM kwa kuwa ni haki ya Kikatiba.
Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi leo Jumanne baada ya Katambi
kuhamia CCM, Dk Mashinji, “sisi kama chama msimamo wetu tuliuweka tangu
madiwani walivyoanza kuondoka, tukaweka msimamo wazi kwamba, suala la
mtu kuondoka kwenye chama au kubaki ni suala la Katiba ya nchi ambayo
inampa mtu uhuru wa kuhama na kwenda kwenye chama anachotakana.”
Amesema kuwa haoni sababu ya kumzuia mtu kuondoka kwa kuwa mtu anapoamua kwenda sehemu yoyote anakuwa na matarajio.
Pia, Dk Mashinji amesema anamtakia heri (Katambi) na kuwataka CCM
kumtumia katika sehemu ambavyo wanaona anafaa kutumika kwa faida ya
Watanzania wote.
“Hatuna mgogoro wowote na kimsingi mimi nimtakie tu heri (Katambi) na
wakipenda (CCM) wamtumie kwenye eneo watakaloona anafaa kutumika kwa
faida ya Watanzania wote,” amesema
Hata Hivyo, Dk Mashinji amesema kuwa walikuwa wanamuandaa Katambi asaidie chama hicho kwenye kitengo cha sheria.
“Alikuwa anamalizia masomo yake ili awe wakili na tulikuwa tumeshaanza
kumuandaa ili atusaidie kwenye kitengo cha sheria ndani ya chama,”
Katambi ametangaza leo kujiunga na CCM mbele ya Mkutano wa Halmashauri
Kuu ya CCM (NEC) unaofanyika katika Ukumbi wa Ikulu jijini Dar es
Salaam.
Na Emmanuel Mtengwa, Mwananchi
