CCM WAKABIDHI MABATI KUKAMILSHA NYUMBA YA MGANGA.
![]() |
Katibu wa Chamaa cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Nicholaus Kasendamila akimkabidhi Mabati 74 mtendaji wa kijiji cha Ikungulyandili Magembe Charles (mwenye shati jeupe) kwa ajili ya kupaulia jengo la mganga katika zahanati ya kijiji hicho, kushoto ni Diwani wa viti maalumu kata ya nkololo Juliana Itabaja. |
Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Nicholaus Kasendamila akimpokea
Mwenyekiti wa kijiji cha Mwasilimbi Ng'ombe Ntemi baada ya kuhamia CCm kutoka
Chadema na kukimvisha kofia na bendera ya CCM, kama ishara ya kupokelewa
NA COSTANTINE MATHIAS,
BARIADI.
CHAMA Cha Mapinduzi
(CCM) wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu kimekabidhi mabati 74 yenye thamani zaidi
ya shilingi 900,000 kwa ajili ya kupaulia nyumba ya Mganga katika zahanati ya
Ikungulyandili.
Akikabidhi msaada huo,
Katibu wa CCM wilayani humo Nicholaus Kasendamila alisema kuwa wanatoa mchango
huo ili kukamilisha ujenzi na pia kuunga mkono nguvu za wananchi waliojenga
boma la nyumba hiyo.
Kasendamila aliwataka
viongozi wa kijiji hicho kuyatumia ipasavyo mabati hayo kama yalivyoelekezwa,
huku akisisitiza juu ya usimamizi wa rasilimali za chama na za serikali.
‘’Baadhi ya viongozi wa
chama na serikali wamekuwa wakihujumu mali za chama kwa kuona kuwa hazina
msimamizi…lakini niwaombe kwa yeyote aliyehujumu mali ya chama hatutasita
kumchukulia hatua’’ alisema Kasendamila.
Akiongea mara baada ya
kupokea mabati hayo, Mtendaji wa kijiji hicho Magembe Charles alimhakikishia
katibu huyo kuwa baada ya siku tatu, watakuwa wamekamilisha kupaua jengo hilo
kwa sababu wameshapandisha kenchi na vifaa vingine vipo.
Katika hatua nyingine
chama hicho kimepokea wanachama wawili ambao ni mwenyekiti wa kijiji cha
Mwasilimbi-Ihusi na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwakitwala-Ihusi waliohama
kutoka chadema kurudi CCM.
Wakiongea mara baada ya
kukabidhi kadi zao walisema kuwa awali walishawishiwa na baadhi ya watu, lakini
kwa sasa wamekuwa hawana msaada kwao wakiwafananisha Chadema na mwindaji
aliyeenda porini na kumwacha mbwa awinde bila kumsaidia.
‘’ Nimeona chama
kimepoteza mwelekeo na hakipo…sawa na mtu aliyesindikiza mbwa kwenda kuwinda
halafu yeye akarudi kulala, nimeamua kuhama mwenyewe na wala sijashinikizwa na
mtu yeyote’’ alisema Ng’ombe Ntemi aliyekuwa Mwenyekiti wa kijiji cha
Mwasilimbi.