Zitto Kabwe: Huu sio Utanzania ni umafia.....Usiku Kucha Sijalala Namuwaza Lissu
Usiku wa kuamkia leo ulikuwa mgumu zaidi kwenye maisha yangu ya kisiasa, anaeleza Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.
“Nimetumia
muda mwingi nikitafakari na kumfikiria sana mwanasiasa mwenzangu, kaka
yangu, mbunge mwenzangu na rafiki yangu Tundu Antiphas Lissu,” amesema
Zitto katika taarifa aliyoitoa leo Ijumaa.
Lissu
alijeruhiwa kwa risasi jana Alhamisi nyumbani kwake Area D mjini Dodoma
na sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Aga Khan mjini
Nairobi, Kenya.
Mbunge
wa Singida Mashariki, Lissu alisafirishwa jana usiku baada ya kupatiwa
matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Zitto
amesema, “Siku zote, katika maisha yetu ya kisiasa, hata katika mambo
tunayotofautiana na kupingana nimekuwa nikiamini kwa dhati kwamba
tofauti hizo haziwezi zikatufanya tukashindwa kuvuka salama kama nchi,
kama Taifa.”
Amesema
kilichotokea kwa Lissu jana Alhamisi ni kitendo cha kihalifu na
kisichoendana na utamaduni wa ustahimilivu na udugu ambao nchi imekuwa
ikisimamia.
“Kitendo
kile cha kikatili kinakwenda kinyume kabisa na misingi ya utaifa wetu
ambao tumekuwa tukiujenga kwa miaka 25 sasa kwa kuwa na taifa huru
kidemokrasia,” amesema.
Amesema Watanzania wanaolitakia mema Taifa wana kila sababu ya kulaani na kukataa utamaduni wa kimafia kuzoeleka nchini.
“Tusimame kulaani kwani #HuuSiUtanzania,” amehitimisha Zitto katika taarifa yake.
