Waziri Simbachawene ajiuzulu kwa agizo la Rais Magufuli
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George
Simbachawene ameandika barua ya kujiuzulu wadhifa huo baada ya kutajwa
katika ripoti za uchunguzi wa biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi
iliyoonyesha namna serikali lilivyopoteza matrilioni ya fedha kutokana
na sababu mbalimbali.
Waziri
Simbachawene ameandika barua hiyo muda mfupi tu tangu Rais Magufuli
alipowataka viongozi wote aliowateua na wametajwa katika ripoti hiyo
wakae pembeni ili kupisha uchunguzi ambao utakuwa huru na wa haki.
Mbali
na Simbachawene, wengine waliokuwa wametakiwa kukaa pembeni ni Naibu
Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani
ambaye alituhumiwa kutotekeleza majukumu yake kikamilifu alipokuwa
akifanya kazi katika Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) lenye dhamana
ya kusimamia madini.
Mbali
na Ngonyani, mwingine ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Eliakim
Maswi naye amepaswa kupisha uchunguzi ambao Rais ameagiza ufanywe na
vyombo vya ulinzi na usalama haraka iwezekanavyo.
Rais
Dkt Magufuli ametoa maagizo hayo leo alipokuwa akipokea ripoti hiyo ya
uchunguzi wa madini kutoka kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye
aliipokea jana kutoka katika kamati zilizoundwa na Spika wa Bunge, Job
Ndugai.
Akiyasema
hayo, Rais Magufuli aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya
uchunguzi kwa wateule wake waliotajwa tajwa katika ripoti hizo lakini
akasema kuwa, uchunguzi hauwezi kufanyika wakati kiongozi akiwa bado
yupo serikali. Baada ya kusema hivyo, Rais Magufuli alisema anaamini
kuwa viongozi hao watakaa pembeni kupisha uchunguzi.
Hafla
hiyo ya kukabidhi ripoti ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Job Ndugai, Wenyeviti wa
kamati mbili za Tanzanite na Almasi, Dotto Biteko na Mussa Azzan Zungu
ambao wote ni wabunge.
Wengine
waliohudhuria ni pamoja na viongozi mbalimbali wa vyombo vya ulinzi na
usalama, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa jumuiya ya wanafunzi
wa elimu ya juu pamoja na viongozi waandamizi wa serikali.
Rais
Magufuli ameendelea kuwasisitiza watanzania kuwa wazalendo kwani
rasilimali za nchini za nchi zinaibiwa na watanzania wanazidi kubaki
katika umasikini uliokithiri.
Baada
ya kuhutubia, Rais Magufuli alikabidhia nakala za ripoti hiyo kwa
viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama ili vianze kufanya kazi mara
moja na sio kuendelea kukaa huku mali za watanzania zikiibiwa.
