WATOTO WENYE UALBINO WAPAKWA RANGI NYEUSI KUWAKINGA
WAZAZI na walezi wenye watoto wenye
ualbino katika Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu wamebuni mbinu mpya ya
kuwapaka rangi nyeusi watoto wao kwenye ngozi na nywele ili kuwalinda
kutofanyiwa vitendo vya ukatili na hata tishio la kuuawa.
Hayo yalisemwa jana na Ofisa Mtendaji wa
Kata ya Dutwa wilayani Bariadi, George Epafra wakati akielezea mbinu
zinazotumika kuwakinga watoto wenye ualbino wakati wa kutambulisha Mradi
wa Kukomesha Mauaji na Albino unaotekelezwa na shirika lisilo la
kiserikali la Mass Media katika wilaya hiyo.
Epafra alisema kwa sasa baadhi ya vituo
vya kulelea watoto wenye ualbino vimefungwa na serikali na watoto hao
kukabidhiwa kwa wazazi wao kwa ajili ya kuendelea kuwalea, hivyo jukumu
la kuwalinda ili wasifanyiwe vitendo vya ukatili limeachwa juu ya wazazi
hao.
“Hivyo watoto wengi sasa wamerudishwa
majumbani na idadi kubwa wako maeneo ya kijijini, hivyo ili wazazi na
walezi wao waweze kuwalinda ili wasije kufanyiwa ukatili pamoja na
kuuawa inabidi wawapake masizi meusi katika sehemu mbalimbali za miili
yao huku nywele zikipakwa dawa aina ya piko zionekane ni nyeusi,”
alieleza.
IMEANDIKWA NA SHUSHU JOEL, BARIADI
