TANZANIA KUNA MAPUNGUFU MAKUBWA KATIKA UTUNZAJI WA KUMBUKUMBU ZA WANAWAKE WALIOCHANGIA MAENDELEO YA TAIFA
Imeeelezwa kuwa sera mbalimbali za kumwezesha mwanamke na kuinua usawa
wa kijinsia nchini haziendani na mazingira ya sasa katika kuelekea
Tanzania yenye viwanda na uchumi wa kati.
Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Mtandao,Vicensia
Shule(pichani) wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu
masuala mbalimbali yaliyojiri wakati wa siku nne za Tamasha la Jinsia
mwaka 2017 lililofanyika katika viwanja vya TGNP Mtandao jijini Dar es
salaam kuanzia Septemba 5 hadi 8,2017.
Alisema miongoni mwa masuala yaliyoibuliwa na washiriki wa Tamasha hilo
katika siku hizo nne ni pamoja na sera za kumwezesha mwanamke kutoendana
na mazingira ya sasa mfano mitaala ya elimu iliyopo haiendani na sera
ya kuelekea Tanzania yenye viwanda na uchumi wa kati.
Alisema washiriki wa tamasha hilo wamependekeza sera zifanyiwe marejeo
ili ziendane na muktadha wa sasa na ziwe na mrengo wa kijinsia.
“Sera hizo pia ziendane na miongozo na mikakati mbalimbali ya kitaifa na
kimataifa kama vile malengo ya maendeleo endelevu,ajenda ya Afrika
2063,Mkataba wa Jinsia na Maendeleo wa SADC,Mpango wa Maendeleo wa miaka
mitano na mpango wa taifa wa kutokomeza ukatili wa kijinsia”,alieleza
Shule.
Katika hatua nyingine alisema ni vyema sasa bajeti kuu za serikali za
mitaa zikazingatia mahitaji ya kijinsia kwa makundi yote huku
akisisitiza kuwa ziwe za kutekelezeka na mchakato wa kuandaa bajeti uwe
shirikishi na wa uwazi bila kujali tofauti za kijiografia,rika,hali ya
uchumi,jinsi,elimu na hali ya ulemavu.
“Utengwaji wa rasilimali pia bado ni changamoto hasa katika kukuza na
kuendeleza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake,mfano ni asilimia
20 ya wanawake Tanzania wanamiliki ardhi”,aliongeza Shule.
Tamasha la Jinsia la 14 mwaka 2017 lililokutanisha washiriki zaidi ya
1500 kutoka ndani na nje ya Tanzania, limehitishwa leo Septemba 8,2017
baada ya siku nne za sherehe,tafakuri,mijadala na pongezi.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Mtandao,Vicensia Shule akizungumza na
waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Ijumaa Septemba 8,2017 katika
ukumbi wa TGNP Mtandao
Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Mtandao,Vicensia Shule akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari
Mkurugenzi Mtendaji TGNP Mtandao,Lilian Liundi akizungumza ambapo
alisema wataendelea kushirikiana serikali pamoja na mashirika mbalimbali
yanayojihusisha na masuala ya kijinsia ili kuhakikisha kunakuwepo na
mageuzi ya mifumo kandamizi kwa usawa wa kijinsia na maendeleo endelevu.

Waandishi wa habari wakiwa ukumbini.
Picha na Kadama Malunde-Malunde1 blog
TAZAMA VIDEO HAPA CHINI.



