YUSUPH MANJI AGOMA KUTUMBULIWA UDIWANI CCM
Mfanyabiashara Yusuf Manji ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo
September 9, 2017 kuwa yeye bado ni Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu na
kudai kuwa hatambui kuvuliwa udiwani kama ilivyotangazwa na Mstahiki
Meya wa Temeke, Abdallah Chaulembo September 6, 2017.
Manji ametoa malalamiko hayo, kwenye kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili
na wenzake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi ambapo katika kesi
hiyo ambayo Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi amedai
upelelezi haujakamilika na Manji kudai ameona habari kupitia gazetini
kuwa amevuliwa udiwani.
Amedai kama ni kweli amevuliwa Udiwani hatambui, kwani ana miezi 2 yupo gerezani na serikali inatambua kwamba yeye ni Diwani.
"Vikao vya awali vya udiwani wa Halmashauri ya Temeke nilikuwa
nahudhuria kwa kuwa naheshimu Mahakama na kwa uzito wa hii kesi sikutaka
kupeleka hata maombi ya dhamana Mahakamani. Mahakama imuagizie DPP na
aiambie Halmashauri ya Temeke kwamba wamenikamata na ndio sababu ya
kutohudhuria vikao. Kama wanataka nihudhurie DPP aombe remove order
nitolewe gerezani ili niende kwenye vikao.”
Pia Manji amedai kuwa kama hilo haliwezekani, basi wamuandikie barua
itakayoonyesha agenda ya vikao vyote na yeye atazijibu kwa njia ya barua
pia.
"Ninachotambua mimi ni Diwani wa Mbagala Kuu na kama nimevuliwa au
sijavuliwa udiwani sitambui. Tayari nimetumia fedha zangu mwenyewe zaidi
ya Tsh. Milioni 70 sio za Halmashauri kwa ajili maendeleo ya wananchi
wake.”
Aidha, amedai kuwa hiyo kesi ni nzito na DPP hapaswi kuangalia upande
wake wa kesi tu, kwani yeye amechaguliwa na wananchi na anawasaidia.
Awali kabla ya kuelezwa hayo, Wakili wa utetezi Seni Malimi alidai kuwa
wanatarajia kuwasilisha maombi ambayo ni ya siri katika tarehe ijayo.
Baada ya kuelezwa hayo, Hakimu Huruma Shaidi akautaka upande wa mashtaka
kuhakikisha wanalifanyia kazi suala hilo, ambapo kesi imeahirishwa hadi
September 18, 2017.
