WAZIRI MKUU AWAONYA WATU WANAOCHUKUA DAWA KATIKA HOSPITALI ZA SERIKALI NA KUZIPELEKA KATIKA MADUKA YAO
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa
amewaonya wamiliki wa maduka ya madawa ya binadamu na watumishi wa sekta
ya afya wanaochukua dawa ambazo zinapaswa kupelekwa katika Hospitali za
Serikali ili kuwahudumia wananchi na kuziweka katika maduka yao.
Mhe. Majaliwa alitoa kauli hiyo jana Wilayani Sikonge katika mkutano wa hadhara na wananchi katika uwanja wa TASAF.
Alisema kuwa vitendo hivyo ndivyo vimekuwa vikisababisha upungufu wa
dawa katika Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali mbalimbali za Serikali
na kufanya baadhi ya wananchi kuendelea kuteseka na maradhi kwa sababu
ya kushindwa gharama za ununuzi wa dawa katika maduka ya watu binafsi.
Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa aliwaonya watumishi wa afya na wamiliki hao
wenye tabia hizo kuacha mara moja endapo watabainika kuendesha vitendo
hivyo watachukuliwa hatua kali.
Alisema kuwa Serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili kununua dawa ili
zinasaidia kutoa huduma ya matibabu kwa wananchi wake lakini kuna baadhi
ya watumishi wa afya wasio waadirifu ambapo wamekuwa wakitorosha dawa
na kuwauzia wamiliki wa maduka ya dawa na ksuababisha upungufu katika
vituo vya Serikali.
Waziri Mkuu kuwa Serikali haiwezi kuwavilimia watumishi wa afya wasio
waaminifu wanaochukua dawa na kuzipeleka katika maduka binafsi huku
wakisababisha upungufu katika baadhi ya hospitali za umma.
Alisema kuwa hospitali ni lazima ziwe na dawa za kutosha ili kuepusha usumbufu kwa wananchi.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu ameikabidhi Kamati ya Ulinzi na
Usalama Mkoa wa Tabora orodha ya watu wenye tabia ya kuwarubuni wakulima
wa tumbaku na kununua katika mfumo ambao si rasmi na kisheria (soko
huria) na kuwanyonya ili wahojiwe.
Alisema kuwa watu hao kwa muda mrefu ndio wamekuwa wakiwanyonya wakulima
kununua tumbaku zao kwa vishanda na kuwa fedha ambazo zinazidi
kuwakandamiza.
“Nina majina ya watu ambao wamekuwa wakipita kwa wakulima na kununua
tumbakuza wakulima kwa njia ya vishada ….huku wakiwanyonya kwa kuwapa
fedha kidogo nawataka waache mara moja.” Alisisitiza Mhe. Waziri Mkuu.
Aliongeza “leo siwataji majina yao lakini nakuachia Mkuu wa Mkoa ili
wewe na Kamati yako ya Ulinzi na Usalama muwaite na kuwahoji na kisha
ziwaonye wasiendelee na biashara hiyo, kama wanataka kuendelea na uuzaji
wa tumbaku wahakikishe wanayopeleka sokoni ni ile waliolima wenyewe na
sio ya kununua kwa wakulima”
Aidha Waziri Mkuu alitoa onyo kwa watumishi wa umma ambao wamekuwa na
tabia ya kugonja wakulima walime tumbaku na wakisha kuvuna na kukausha
wao wanakwenda kununua kwa ajili ya kuipeleka katika makampuni ya
tumbaku.
Alisema mtumishi hakatazwi kulima kulima tumbaku bali atakiwi kununua tumbaku kutoka kwa mkulima.
Waziri Mkuu huyo aliwaagiza viongozi wa Mkoa wa Tabora kukamata watu
wote wanajihusisha na ulanguzi wa tumbaku ya wakulima na kuongeza kuwa
watakamatwa wakiwa na tumbaku ya ulanguzi ichukuliwe pamoja na chombo
cha usafiri kinachotumika kusafirishia.
Alisema kuwa tumbaku yote inauzwa kupitia vyama vya msingi na kila mtu atauza tumbaku kwa kiwango alicholima.
Na Tiganya Vincent-RS-Tabora
