Wakimbizi 6,700 raia wa Burundi wajiandikisha kurejea makwao kwa Hiari
Mwandishi Wetu – MAELEZO
Kufuatia
wito wa Rais John Pombe Magufuli alioutoa hivi karibuni, hadi kufikia
tarehe 01 Agosti, 2017 jumla ya wakimbizi 6,700 raia wa Burundi
wameshajiorodhesha kurejea nchini mwao kwa hiari.
Kufuatia
hatua hiyo, Mkutano wa pande tatu utakaojumuisha Serikali za Tanzania,
Burundi na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) unatarajiwa kufanyika
mwishoni wa mwezi huu kujadili namna ya kuwarejesha nchini mwao
wakimbizi hao kwa kuzingatia sheria za kimataifa zinazohusu wakimbizi.
Katika
mahojiano na mwandishi wetu ofisi kwake jana, Mkurugenzi Idara ya
Huduma za Wakimbizi katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bwana
Harrison Mseke alieleza kuwa tangu kutolewa kwa wito huo, Wizara imekuwa
ikiwamahasisha wakimbizi hao kujiorodhesha kwa hiari ili waweze kurejea
nyumbani.
Akiwa
katika ziara yake kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa, Rais Magufuli alitoa
wito kuwataka wakimbizi raia wa Burundi kurejea nyumbani kwa hiari kwa
kuwa hali ya usalama nchini mwao ni nzuri ambapo wakati akitoa wito huo
tarehe 20 Julai, 2017 huko Ngara aliambatana na Rais wa Burundi, Pierre
Nkurunzinza ambaye nae aliwahakikishia wakimbizi hao kuwa hali ni shwari
nchini Burundi.
Kwa
mujibu wa Bwana Mseke, hivi sasa kuna wakimbizi raia wa Burundi 276,692
kati ya wakimbizi 348,019 walioko nchini. Wengine ni wakimbizi kutoka
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) 70,840, Wasomali 150, na wengine
(mchanganyiko) 337.
Alifafanua
kuwa kati ya idadi hiyo ya wakimbizi raia wa Burundi 242,340 waliingia
nchini baada ya mwezi Aprili, 2015 kufuatia machafuko ya kisiasa nchini
humo.
Akizungumzia
mwendo wa uingiaji wakimbizi kutoka Burundi, alieleza kuwa kwa sasa
kasi imepungua kutoka wastani wa wakimbizi 1,000 kwa siku kati ya mwezi
Agosti hadi Disemba, 2016 hadi wastani wa wakimbizi kumi kwa siku katika
miezi ya hivi karibuni.
“Mwezi
Januari mwaka huu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alifuta tamko la
Primafacie alilolitoa mwezi Mei, 2015 ambalo linataka wakimbizi
wanaokimbia machafuko nchini kwao waruhusiwe kuingia kwa makundi bila ya
utambuzi,” alieleza Bwana Mseke.
Alibainisha
kuwa, bila ya tamko hilo “Kwa wastani wa wakimbizi 1000 kwa siku
kuanzia Januari, 2017, tungekuwa tunapokea wastani wa wakimbizi 30,000
kwa mwezi na hadi kufikia sasa tungekuwa tumepokea wakimbizi wapatao
240,000”.
Aliongeza
kuwa hatua hiyo ya Waziri kufuta tamko hilo ilizingatia hali halisi ya
utulivu na usalama nchini Burundi ambapo ilikuwa imetengamaa na maisha
yamerejea katika hali ya kawaida.
Mkurugenzi
huyo wa Huduma za Wakimbizi alieleza kuwa raia wa Burundi ambao
walikuwa wakiingia nchini mwaka jana wengi walikuwa wakikimbia hali ya
upungufu wa chakula nchini humo tatizo ambalo lilizikumba pia baadhi ya
nchi nyingine katika ukanda huu.
Wakati
akitoa wito huo, Rais Magufuli aliiagiza pia Wizara ya Mambo ya Ndani
ya Nchi kusitisha mara moja kuwapatia uraia wakimbizi raia wa Burundi.
Bwana
Mseke alibainisha kuwa serikali tangu Awamu ya Kwanza imekuwa
ikiwapatia uraia wakimbizi kutokana na hali halisi ambapo mwaka 1983
wakimbizi 32,000 raia wa Rwanda walipewa uraia. Kati ya mwaka 1995 na
2012 wakimbizi wa kisomali wenye asili ya kibantu 3,000 walipewa uraia
na mwaka 2014 wakimbizi raia wa Burundi 162,156 walipewa uraia.
Agizo
hilo la Rais la kusitisha utoaji uraia kwa wakimbizi linatarajiwa
kusaidia kupunguza idadi ya wakimbizi nchini kwa kuwa imeibainika baadhi
yao huja nchini kwa nia ya kujipatia uraia.