Taarifa Toka Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais IKULU
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
amesema Serikali imeanza kuchukua hatua dhidi ya watu waliouziwa
mashamba makubwa Mkoani Tanga na kisha kuyatelekeza ambapo mpaka sasa
hati miliki za ardhi 5 zenye zaidi ya ekari 14,000 zimefutwa.
Mhe.
Rais Magufuli amesema hayo jana tarehe 03 Agosti, 2017 kwa nyakati
tofauti wakati akizungumza na wananchi wa Mkata, Komkonga, Kabuku,
Michungwani, Hale, Muheza na Pongwe katika Wilaya za Handeni, Muheza na
Tanga ambako ameanza ziara ya kikazi ya siku 5 Mkoani wa Tanga.
Mhe.
Rais Magufuli alifafanua kuwa Mkoa wa Tanga una mashamba 72 yaliyouzwa
kwa watu mbalimbali na kwamba hatua za kunyang’anya mashamba
yaliyotelekezwa zimeanza kuchukuliwa kwa mashamba 12 na tayari mashamba 5
ambayo hati zake zimeshafutwa, utaratibu unaendelea kuwagawia wananchi
na wawekezaji watakaokuwa tayari kuyaendeleza kama ilivyokusudiwa.
Sambamba
na hilo akiwa Mkata Wilayani Handeni, Mhe. Dkt. Magufuli ameagiza
shamba la ekari 50 lililopo katika kijiji cha Kabuku na ambalo
lililotolewa na wananchi kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa lengo la
kujenga kiwanda miaka 7 iliyopita, lirejeshwe kwa wananchi na ametaka
JKT ijenge kiwanda hicho katika eneo lake jingine lenye ukubwa wa zaidi
ya ekari 9,000.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli ametoa siku 15 kufanyika kwa uchunguzi wa fedha
kiasi cha Shilingi Milioni 500 zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa
majengo ya kituo cha afya cha Mkata, kufuatia kuwepo kwa taarifa za
ufujaji wa fedha hizo na ameongeza kuwa Serikali itapeleka Shilingi
Milioni 800 kwa ajili ya kuendeleza kituo hicho baada ya hatua stahiki
kuchukuliwa.
“Siku
15 tuwe tumepata jibu ili fedha nyingine Shilingi Milioni 800 zije,
kama huyo Mkandarasi hafai afukuzwe, kama kuna mtu hafai aondolewe,
tuanze na ukurasa mpya, na ningeomba Mkuu wa Wilaya ulifuatilie hili ili
asiponyoke mtu yeyote, na wewe una Mamlaka yote” alisema Mhe. Rais Magufuli.
Kuhusu
maji, Mhe. Rais Magufuli alisema Serikali imeanza kuchukua hatua dhidi
ya tatizo hilo ikiwemo kutoa Shilingi Bilioni 2 kwa ajili ya kuupatia
maji Mji wa Muheza na vijiji vingine na kwamba mradi mwingine wa
Shilingi Bilioni 30 utatekelezwa ili kumaliza tatizo hilo.
Mhe.
Rais Magufuli aliwataka wananchi wa Tanga kujipanga kunufaika na fursa
mbalimbali za ajira na biashara kufuatia mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba
la mafuta ghafi la kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga
hapa Tanzania na amewahakikishia kuwa mradi huo utatoa mchango mkubwa
katika maendeleo ya Tanga na Taifa kwa ujumla.
“Ndugu
zangu wananchi wa Tanga nataka kuwahakikishia kuwa tunakwenda vizuri,
tumepata mradi huu mkubwa na pia uchumi wetu unakwenda vizuri, hivi sasa
nchi yetu ni kati ya nchi 5 duniani zenye uchumi unaokua kwa kasi na ni
nchi ya 2 barani Afrika ikitanguliwa na Ethiopia” alisisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Katika
ziara hii Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli,
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy
Mwalimu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
Mhe. Januari Makamba na Wabunge wa Mkoa wa Tanga.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Tanga