JINSI RAIS MAGUFULI ALIVYOIBUKIA FERI DAR
RAIS
John Magufuli jana alifanya ziara ya kushtukiza katika eneo la Feri na
kisha kuvuka bahari kwa kutumia kivuko cha MV Kigamboni ambako alikutana
na wananchi wa Kigamboni, kutembelea Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu
Nyerere na alitembelea Daraja la Nyerere la Dar es Salaam.
Baada ya kukata tiketi, Rais Magufuli alipata wasaa wa kuzungumza na
wananchi aliosafiri nao katika kivuko cha MV Kigamboni na baadaye
kuzungumza na wananchi wa Kigamboni ambapo aliulizwa na kujibu mambo
mbalimbali. Kuhusu ubovu wa barabara, Rais Magufuli alisema serikali
imechukua hatua ya kukabiliana na tatizo hilo kwa kuanzisha Wakala wa
Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) ambayo itafanya kazi ya kutengeneza
barabara kwa kiwango cha lami.
Kuhusu tatizo la kukatika kwa umeme alisema Serikali inatekeleza miradi
mbalimbali itakayoongeza kiwango cha umeme katika gridi ya taifa pamoja
na kurekebisha miundombinu yake na amewaomba kuwa na subira wakati
juhudi hizo zinaendelea. Akiwa katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu
Nyerere, Rais Magufuli alikutana na vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kutoka vyuo na vyuo vikuu vya Mkoa wa Dar es Salaam waliopiga kambi
katika chuo hicho, ambao wamempongeza kwa kazi kubwa na nzuri
anayoifanya kuiongoza Serikali ya Awamu ya Tano ambayo kwa muda mfupi
imeonesha uongozi unaoacha alama.
Vijana hao walimhakikishia kuwa wanamwunga mkono na walimwahidi kuwa
wapo tayari kuitumikia nchi kwa jukumu lolote watakalopewa na kwamba
daima watatanguliza maslahi ya nchi. Akizungumza na vijana hao, Rais
Magufuli aliwapongeza kwa moyo wa uzalendo waliouonesha, na aliwataka
kuwa nguzo imara ya mabadiliko ya kweli nchini ili juhudi zinazofanywa
na Serikali ya Awamu ya Tano kurekebisha mambo yaliyosababisha kukiuka
misingi ya waasisi wa Taifa zizae matunda.
Alieleza baadhi ya juhudi hizo kuwa ni kukabiliana na rushwa
inayodhoofisha uchumi na huduma za kijamii, kudhibiti mianya ya matumizi
mabaya na upotevu wa fedha na mali za umma na kuondoa watumishi hewa na
wenye vyeti vya kughushi. Juhudi nyingine ni kuongeza bajeti ya
maendeleo katika bajeti ya Serikali, kuongeza uzalishaji wa umeme,
kujenga viwanda, kujenga reli, kununua ndege za Serikali, kuongeza
ukusanyaji wa kodi na kuchukua hatua kali dhidi ya wahujumu uchumi.
“Nataka niwahakikishie vijana wote kuwa nawapenda sana, hata mimi
nilikuwa Umoja wa Vijana, yote yaliyotokea kinyume na misingi ya chama
hiki na misingi ya waasisi wetu wakiongozwa na Mwalimu Nyerere nimeamua
kuyanyoosha na yatanyooka, na nyinyi simameni imara, kitumikieni chama
na msitumikie watu au vikundi vya watu, mkifanya hivyo kila kitu
kitakwenda vizuri kabisa,” alisisitiza Rais Magufuli.
Aliwataka vijana hao kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi
katika uchaguzi wa chama utakaofanyika baadaye mwaka huu, na alibainisha
kuwa wasiwe na hofu ya kuwepo kwa rushwa kwa kuwa wote watakaojihusisha
na vitendo vya rushwa hawatapitishwa kuwania nafasi za uongozi ndani ya
chama.
Pia aliwaambia viongozi wa Sekretarieti ya CCM aliowakuta wakizungumza
na vijana hao kuwa anazo taarifa zote juu ya watu waliojimilikisha mali
za chama na alisema anasubiri wakati ukifika achukue hatua
zinazostahili. Baada ya kuzungumza na vijana hao, Rais Magufuli
alitembelea Daraja la Nyerere na kuzungumza na wananchi wa eneo hilo,
ambapo alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kufanyia
kazi ombi la wananchi kujengewa kituo cha daladala.
Via>>Habarileo