HABARI SHINYANGA SIASA MICHEZO BURUDANI MAPENZI MAGAZETI NYIMBO ZA ASILI POLISI SINGIDA WAUA MTU MMOJA ANAYEDAIWA KUWA NI JAMBAZI
Mkazi wa kijiji cha Shiponga, Hanang Mkoani Manyara anayedaiwa kuwa
jambazi, Hamisi Athumani (32), amefariki dunia baada ya kupigwa risasi
kiunoni na askari polisi wakati akiwa katika harakati ya kutoroka.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani hapa, ACP Debora Magiligimba, amesema
tukio hilo limetokea Agosti 25 mwaka huu saa nane mchana, huko katika
kijiji cha Mgori tarafa ya Ngimu wilaya ya Singida.
Amefafanua kuwa Hamisi (marehemu) alipigwa risasi na askari polisi
wakati akijaribu kuwatoroka mara baada kuonyesha bunduki aina ya rifle
yenye namba 7358 na risasi zake tano.
Amesema bunduki hiyo iliyokuwa imekatwa mtutu na risasi zake tano
zilikuwa zimefichwa kwenye soksi, vitu hivyo vilikuwa vilihifadhiwa
kwenye mfuko wa sandarusi, na kufichwa chini ya jiwe.
ACP Magiligimba amesema Agosti 23 mwaka huu, mtuhumiwa alikamatwa na
wananchi wa kijiji cha Ngamu, na kufikishwa katika kituo cha polisi cha
kijiji hicho kwa tuhuma ya kujihusisha na matukio ya ujambazi.
“Kesho yake mtuhumiwa alihojiwa na kukiri kujihusisha na matukio ya
ujambazi wa kutumia silaha katika mikoa mbalimbali. Pia aliahidi
kuwapeleka askari kuwaonyesha mahali alikoificha silaha anayoitumia
kwenye matukio hayo ya ujambazi,” amesema ACP Magiligimba.
Kamanda huyo amesema Agosti 25 mwaka huu saa sita mchana, askari polisi
wakiwa na mtuhumiwa, walikwenda katika pori la kijiji cha Mgori mahali
alipokuwa ameficha bunduki hiyo aina ya rifle.
“Mara tu baada ya kuwaonyesha askari hao silaha hiyo na wakati askari
wanaendelea kufanya upekuzi katika eneo hilo, mtuhumiwa alijaribu
kutoroka askari kwa kukimbia” amesema na kuongeza.
“Askari mmoja alifyatua risasi tatu hewani akimtaka asimame, lakini
hakutii. Ndipo alipompiga risasi moja iliyompata sehemu ya kiunoni”.
Amesema jereha hilo la risasi lilisababisha mtuhumiwa Hamisi avuje damu
nyingi, na hivyo kufariki dunia wakati akikimbizwa hospitali ya mkoa kwa
matibabu.
“Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida linaendelea kutoa wito kwa wananchi
waote kutoa taarifa zitakazosaidia kubaini wahalifu katika maeneo yao
ili hatua ziweze kuchukuliwa kudhibiti vitendo vya kihalifu,” amesema
kamanda huyo.