Cuba kumaliza uhaba wa sukari Tanzania
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Shirika
la Viwanda vya Sukari nchini Cuba, Bw. Francisco Lled, ambaye amekubali
kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuongeza uzalishaji wa
sukari nchini.
Shirika
la Sukari la nchini Cuba linauwezo wa kuzalisha tani milioni nne za
sukari kwa mwaka huku mahitaji ya ndani ni tani 700,000, ambapo kiasi
kinachobaki huuzwa nje ya nchi. Kwa sasa shirika hilo linazalisha tani
milioni mbili tu katika viwanda vyake 56.
Waziri
Mkuu alikutana na Bw. Lled Alhamisi, Agosti 24, 2017, wakati alipofanya
ziara katika kiwanda cha kuzalisha sukari cha UGB Central Azucarero 30
de Noviembre katika mji wa San Nicola’s de Bari ambacho ni kati ya
viwanda 27 vya shirika hilo linalomilikiwa na Serikali ya Cuba kwa
asilimia 100.
Katika
mazungumzo yao Waziri Mkuu alimshawishi Bw. Lled kuja nchini kwa ajili
ya kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha sukari. Alisema kwa
sasa Tanzania kuna viwanda vikubwa vitano vya sukari ambavyo uzalishaji
wake hautoshelezi mahitaji ya ndani.
Waziri
Mkuu alivitaja viwanda hivyo ambavyo ni Mtibwa na Kilombero (Morogoro),
Mahonda (Zanzibar), TPC (Kilimanjaro) na Kagera ambavyo vyote
vinazalisha jumla ya tani 320,000 za sukari kwa mwaka huku mahitaji
yakiwa ni zaidi ya tani 400,000.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu alisema Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi
inatarajia kujenga viwanda vitatu vya kuzalisha sukari, ambavyo
vitazalisha sukari itakayotosheleza mahitaji na ndani ya nchi na kiasi
kitakachosalia kitauzwa nje.
Kwa
upande wake Bw. Lled alisema sera za Cuba haziruhusu shirika kwenda
kuwekeza nje ya nchi na badala yake wanaruhusiwa kuzisaidia nchi
zinazohitaji kujenga viwanda hivyo kwa kutoa ushauri na usimamizi wa
ujenzi wa miradi hiyo.
Alisema
Shirika lake lipo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika
usimamizi na kutoa ushauri wa ujenzi wa miradi ya viwanda vya kuzalisha
sukari na kwamba walishatoa huduma kama hiyo katika nchi mbalimbali
zikiwemo Brazil na Bolivia.
Katika
hatua nyingine, Bw. Lled alisema mbali na uzalishaji sukari pia shirika
hilo kupitia viwanda vyake vya sukari wanazalisha vyakula vya mifugo,
asali ambayo inatumika katika viwanda vya kutengeneza vinywaji vikali
pamoja nishati ya umeme.
Alisema
miwa ya kuzalishia sukari katika viwanda vyao wanaipata kutoka kwenye
vikundi vya ushirika wa kulima wa miwa vilivyoko katika mikoa yote nchi
nzima kasoro mkoa wa Havana na Pañar del Rio na kwa mkulima mmoja mmoja
ambao kwa pamoja hukusanya miwa katika vituo ambavyo hupeleka kiwandani.
Hata
hivyo alisema kuwa viwanda vyao vinanunua miwa kwa bei tofauti
kulingana na ubora wa miwa na kwamba shirika lao linawasaidia wakulima
kwa kuwaelimisha namna bora ya kulima pamoja na kuwaazima mashine za
kuvunia wakati wa mavuno. Miwa yote nchini Cuba inavunwa kwa kutumia
mashine.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAAA, AGOSTI 25, 2017.