Yusufu Manji Asomewa Mashitaka 7 Akiwa Muhimbili
Mfanyabiashara
Yusuf Manji na wenzake watatu jana wamesomewa mashtaka saba katika
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyoko ndani ya Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) ambako mahakama ilihamia jana kwa muda.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuhamia hospitalini hapo, alikolazwa Manji.
Manji
(41) na wenzake, wanadaiwa kukutwa na vitambaa vyenye thamani ya Sh200
milioni, vinavyotumika kutengeneza sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ). Pia, wanadaiwa kukutwa na mihuri.
Wanashtakiwa chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Sheria ya Usalama wa Taifa.
Washtakiwa wengine ni Deogratius Kisinda (28), Abdallah Sangey (46) na Thobias Fwere (43).
Walisomewa
mashtaka hayo ndani ya wodi aliyolazwa Manji na wakati yakisomwa, Manji
alikuwa amevaa sare za bluu za wagonjwa na alikuwa ameketi kitandani
huku mkononi akiwa ametundukiwa dripu.
Wenzake walisimama pembezoni mwa kitanda chake.
Mbele
ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, Wakili wa Serikali, Tulumanywa
Majigo, alidai Juni 30 katika eneo la Chang’ombe A wilayani Temeke, Dar
es Salaam, washtakiwa kwa pamoja walikutwa na askari polisi wakiwa na
mabunda 35 ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za JWTZ zenye
thamani ya Sh192.5 milioni na kwamba, mali hiyo ilipatikana kinyume cha
sheria.
Katika
shtaka la pili, alidai Julai Mosi katika eneo hilo, walikutwa na polisi
wakiwa na mabunda manane ya vitambaa hivyo yenye thamani ya Sh44
milioni mali ambayo ilipatikana isivyo halali.
Washtakiwa
katika shtaka la tatu wanadaiwa Juni 30 katika eneo hilo, walikutwa na
muhuri wenye maandishi Mkuu 121 kikosi cha JWTZ bila kuwa na uhalali,
kitendo ambacho kingehatarisha usalama wa nchi.
Majigo
katika shtaka la nne, anadai Juni 30 eneo la Chang’ombe A, walikutwa
wakiwa na muhuri wenye maandishi Kamanda 834KJ Makutupora, Dodoma bila
kuwa na uhalali, kitendo ambacho kingehatarisha usalama wa nchi.
Shtaka
la tano, wanadaiwa Juni 30 katika eneo hilo walikutwa na muhuri wenye
maandishi, Commanding Officer 835KJ Mgambo P.0. Box 224 Korogwe bila
kuwa na uhalali.
Katika
shtaka la sita, wanadaiwa Julai Mosi katika eneo hilo walikutwa na
askari polisi wakiwa na namba ya usajili wa gari SU 383 ambayo
ilipatikana kwa njia isiyo halali.
Washtakiwa
katika shtaka la saba, wanadaiwa Julai Mosi kwenye eneo hilo walikutwa
na askari polisi wakiwa na namba ya usajili wa gari SM 8573, ambayo
ilipatikana kwa njia isiyo halali.
Baada
ya kusomewa mashtaka, hawakutakiwa kuzungumza chochote kwa sababu
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo
na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hakuwasilisha hati ya kuipa mamlaka
mahakama hiyo kuisikiliza.
Pia, upande wa mashtaka uliwasilisha hati kutoka kwa DPP ya kuzuia dhamana kwa washtakiwa.
Mawakili
wa utetezi, Hudson Ndusyepo, Malimi Seni na Emmanuel Safari walipinga
hati ya kuzuia dhamana wakiiomba mahakama isiipokee kwa sababu haina
mamlaka na kesi hiyo.
Walidai kitendo cha DPP ni matumizi mabaya ya madaraka na hawatendi haki kwa washtakiwa.
Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 19, kwa ajili ya kutajwa.