Waziri Mpango Awatuliza Machinga Nchini
Benny Mwaipaja, WFM-Dar es Salaam
Waziri
wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amewahakikishia wafanyabiashara
wadogo maarufu kama wamachinga kwamba Serikali itaendelea kuwawekea
mazingira mazuri ya kufanyia biashara zao ili waweze kujikwamua
kiuchumi.
Dkt.
Mpango ametoa kauli hiyo baada ya kukagua zoezi la usajili wa
wafanyabiashara hao linaloendelea katika katika Ofisi za TRA wilaya ya
Ilala Jijini Dar es Salaam ambapo ameshuhudia idadi kubwa ya
wafanyabiashara hao wakiwemo waendesha bodaboda, mamalishe na wauza
bidhaa mbalimbali wakiendelea kujisajili ili wapate vitambulisho.
“Ndio
maana tumeona tuweke utaratibu wa kuwaandikisha na tuwapatie
vitambulisho hatimaye tuweke mpango maalumu wa kuwapatia maeneo rasmi ya
kufanyiabiashara zenu badala ya kila siku kuwatumia askari mgambo
kuwafukuza wakati mnatafuta riziki,” alisema Dkt. Mpango.
Amesema
lengo la kufanya hivyo ni kuwawekea wafanyabiashara hao wadogo
utaratibu mzuri ii waendelee kufanya kazi zao za kujenga familia na
Taifa kwa ujumla bila bughudha kwa kuwa Serikali inathamini mchango wao
katika uchumi na maendeleo ya nchi.
“Ni
lazima ifike mahali kila mtanzania achoke na umasikini, na sisi
Serikali yenu tufanyekazi ya kuwasaidia kujikwamua kiuchumi badala ya
kuwakandamiza,” aliongeza Dkt. Mpango
Dkt.
Mpango amesema nchi ya Sweden imeweka utaratibu mzuri wa masoko maalumu
kwa ajili ya wamachinga wao kila siku za Jumamosi na Jumapili ambapo
watu wengi hufika maeneo hayo kununua bidhaa hali inayoashiria kuwa
suala la uwepo wa wafanyabiashara wadogo wadogo ni la nchi nyingi
duniani.
“Nawasihi
mkawaeleze Watanzania wengine na wafanyabiashara ndogo ndogo wenzenu
wajitokeze kwa wingi kujiandikisha ili wasajiliwe na kupewa vitambulisho
vitakavyowasaidia kujulikana,” alisisitiza Dkt. Mpango
Amerejea
kauli yake ya kuwapongeza Watanzania wote kwa niaba ya Rais Dkt. John
Magufuli kwa kujitokeza kwa wingi kulipa kodi mbalimbali ikiwemo kodi ya
majengo kwa kuwa kodi hizo zinaipa Serikali nguvu na uwezo wa
kuwahudumia ipasavyo.
Mkiona
barabara zinajengwa, tunaboresha huduma za afya kwa nunua dawa za
kutosha, mjue kuwa kodi yenu hiyo kidogo kidogo mnayotoa ndiyo
inayotumika kuwezesha mambo hayo kufanyika (makofi)†Alisisitiza
Waziri huyo wa Fedha na Mipango
Dkt.
Mpango ameahidi kutatua changamoto ya upungufu wa watumishi na
vitendeakazi katika kituo hicho cha uandikishaji ama usajili wa
wafanyabishara wadogo wadogo kilichoko katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato
Tanzania-TRA, Ilala Jijini Dar es Salaam ili kufanikisha kazi hiyo.
Kwa
upande wao, wafanyabiashara wadogo wadogo hao wameipongeza Serikali kwa
hatua waliyoichukua ya kuwatambua rasmi na kuwaingiza katika mfumo wa
ulipaji kodi kwa maendeleo ya nchi.
Wamemwomba
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango awafikishie salamu zao
za dhati kwa Mhe. Rais Dkt. John Magufuli, kwamba wanamuunga mkono
katika jitihada zake za kuwaletea wananchi maendelo na kupambana na
vitendo vya rushwa na ufisadi pamoja na kujenga nidhamu ya watumishi wa
umma na matunda yake yameanza kuonekana katika uwajibikaji.