Waziri Mkuu Atembelea Mradi Wa Kusafirisha Umeme Lindi.......Asema changamoto ya kukatika umeme Mkoa wa Lindi kuwa historia
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
changamoto ya kukatika umeme katika mkoa wa Lindi kuwa historia baada ya
kukamilika kwa mradi wa kusafirisha umeme wa kilovolti 132
Mtwara-Lindi.
Amesema
hayo jana (Alhamisi, Julai 13, 2017) alipotembelea mradi huo wa
kuzalisha umeme unaojengwa katika kijiji cha Mahumbika wilayani Lindi.
Waziri
Mkuu alisema kukamilika kwa mradi huo uliogharimu sh. bilioni 16
kutamaliza changamoto ya upatikanaji wa umeme katika mkoa wa Lindi.
Alisema
mkakati wa Serikali ni kuongeza kiwango cha uzalishaji wa umeme ili
Watanzania wapate umeme mwingi utakaosambazwa hadi vijijini kwa gharama
nafuu.
“Mikoa
wa Lindi ulikuwa na shida kubwa ya kukatika kwa umeme, kukamilika kwa
mradi huu ni mkombozi kwetu, tunawakaribisha wawekezaji waje kuwekeza
kwa sababu sasa tunanishati ya uhakika.”
Kwa
upande wake Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa
James Mdoe alisema kuimarika kwa upatikanaji wa umeme kutawezesha safari
ya kuelekea kwenye uchumi wa viwanda.
Katika
hatua nyingine Waziri Mkuu amesema atahakikisha anapambana na watu wote
watakaokwamisha jitihada za Rais Dkt. John Magufuli za kuwahudumia
wananchi.
Pia
ameahidi kusimamia shughuli za maendeleo ya wananchi wote Tanzania bila
ya kujali maeneo wanakotoka wala itikadi zao za kisiasa na kidini.
Ameyasema
hayo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa kata za
Nanganga, Nyangao, Mtama na Nyengedi alipowasilisi wilayani Lindi, akiwa
katika ziara yake ya kikazi mkoani Lindi.
“Tunataka fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kuwahudumia
wananchi zitumike ipasavyo na hatutakubali kuona mtu napewa fedha na
kuzitumia atakavyo.”
Pia
Waziri Mkuu amewataka wananchi hao kuweka pembeni itikadi zao za
kisiasa na badala yake washirikiane kwa pamoja katika kufanya shughuli
za maendeleo kwenye maeneo yao.
“Rais
Dkt. Magufuli amesema Watanzania kwa sasa hatuhitaji kufanya siasa,
sasa ni kazi tu, hivyo tutumie muda wetu mwingi kwa kufanya kazi za
maendeleo. Tupunguze muda wa kubishana hakuna tija watu wanataka maji,
afya.”
Awali
Mbunge wa jimbo la Mtama Mheshimiwa Nape Nnauye kwa niaba ya wananchi
wa jimbo hilo aliishukuru Serikali kwa kuboresha huduma mbalimbali
kwenye jimbo hilo.