Waziri Lukuvi Aonya Maafisa Ardhi Wasio Waadilifu
Na Hassan Mabuye Kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Ardhi
Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amewaonya
maafisa ardhi na maafisa mipango miji wasio waadilifu na kusababisha
kero za migogoro ya ardhi nchini.
Waziri
Lukuvi aliyasema hayo jana katika ukumbi wa shule ya sekondari
Lugalo mjini Iringa wakati wa Uzinduzi wa Master Plan ya
Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.
Alisema
mchezo huo wa ufisadi ambao umekuwa ukitumiwa miaka yote na maofisa
ardhi nchini ameubaini na kuwataka wakurugenzi wa Halmashauri nchini
kutokubaliana na ramani za maeneo mapya zinazoletwa na wataalam hao
bila ya wao kufika maeneo husika na kuoneshwa maeneo hayo ili
kujiridhisha.
Waziri
Lukuvi alifichua kuwa ufisadi unaofanywa na maafisa ardhi nchini kwa
kupima viwanja hewa kwa ajili ya maslahi yao na kusema kuwa mbinu
ambayo wamekuwa wakiitumia kuiibia serikali amekwisha ibaini na
hata kubali kuona mbinu hiyo inapewa nafasi katika serikali hii ya
awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli .
Maafisa
ardhi wakishirikiana na maafisa mipango miji pamoja na wapimaji
wamekuwa wakitajirika sana kwenye idara zao na wanatakata kwa
ujanjaujanja na ufisadi wanaoufanya kwa kutengeneza ramani
zinazoonesha maeneo mazuri na muhimu katika miji kwamba hayafai
kutumika, kumbe wameyauza maeneo hayo kwa mlango wa nyuma na kwa bei za
juu.
Unakuta
kwenye ramani inayonyesha kuna bonde kubwa lisilofaa kujengwa
kumbe ukifuatilia eneo hilo ni zuri kuliko yote na hapo wametenga
viwanja vya kuuza. Unakuta ukipima kuna viwanja vingi na vizuri
ambavyo ni vyao wao wanachofanya baada ya kuuza viwanja halali za
Halmashauri hurudi kupima maeneo hayo walioonyesha ni mabonde na
kugawana wao kwa ajili ya kuuza kwa faida yao.
Lukuvi
alisema kuwa wathamini nao pi wamekuwa wakiwapunja wananchi wasio
elewa kwa kuwafanyia tathimini kubwa zaidi ya uhalisia wake na
pindi pesa inapotoka utakuta nyumba inathamani ya milioni 7 wakati wao
wanasema inathamani ya milioni 20 ili cha juu wapate wao.
“wakati
nilipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam niliweza kubaini ujanja wa
wathamini baada ya eneo ambalo nyumba zake zina thamani kati ya
milioni 20 hadi 50 kwa maana nyumba hizo ni za udongo ila maofisa
hao walimtafuta mtu na kutafuta nyumba nzuri zaidi na kumshikisha
kibao kisha kumpiga picha na kuandika kuwa nyumba hiyo inathamani
ya zaidi ya milioni 200.
"Niliamua
kufanya uchunguzi wangu na kumtafuta mtu aliyekwenye picha na kumbana
ndipo aliniambia ukweli kuwa mthamini huyo ni ndugu yake hivyo
walikubaliana pesa ikitoka atalipwa milioni 70 na milioni 130 ni za
afisa huyo”
Hata
hivyo alisema kuwa ujenzi holela katika miji na halmashauri
imesababishwa na ukilitimba wa utoaji wa vibali kwa wakati na ndio
sababu ya wananchi kuvamia maeneo yasiyo pimwa japo kuanzia sasa
wote waliopo katika maeneo yasiyo pimwa watapewa leseni ya makazi ya
miaka mitano na watalipa kodi ya ardhi na baada ya miaka mitano
wahakikishe wamepimiwa ili kupewa hati.
Hivyo
Lukuvi aliwataka maafisa ardhi na wathamini wa ardhi manispaa ya
Iringa kutofanya kama maeneo mengine kwa kufuata mpango maeneo yote
ambayo yameelekezwa kwenye Masta Plan hiyo na kwenda kutenda haki.
Katika
hatua nyingine waziri Lukuvi alitoa agizo kwa wale wote
waliopewa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa hoteli na viwanda na wale
waliouziwa viwanda vya serikali, hotel na mashamba ya serikali
kuviendeleza haraka kabla ya ardhi hiyo haijapokonywa .
Nae
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bibi Amina Masenza akimkaribisha waziri
Lukuvi alsema kuwa mkoa wa Iringa umeendelea kuhamasisha wananchi
kuzingatia sheria na taratibu za ujenzi na kuachana na ujenzi holela
na ndio sababu ya kuja na Masta Plan hiyo ambayo imeanzishwa na
aliyekuwa mstahiki meya wa halmashauri hiyo Amani Mwamwindi.
Akitoa
taarifa ya uandaaji wa Masta Plan hiyo kwa ajili ya mwaka 2015-2035
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Dkt William Mafwere,
alisema kuwa dhumuni la mpango huo ni kutatua changamoto zilizokuwa
zinaikabili Manispaa na kuwa dhana kuu ya mpango huo ni dhana unganishi
ikijumuisha dhana nyingine.
Alisema
jumla ya miradi 31 itatekelezwa katika awamu ya kwanza 2015-2020 kuwa
baadhi ya miradi hiyo ni kituo cha mabasi Igumbilo, kituo hicho kimeanza
ujenzi na hatua ya utekelezaji imefikia asilimia 30.
Nae
Mbunge wa jimbo la Iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa alisema kuwa
kazi inayofanywa na Waziri Lukuvi ni tofauti na mawaziri wengine
kwani amekuwa ni waziri wa mfano katika kuchapa kazi.
“Kwa
mnaonifahamu vizuri mimi sio mbunge wa kusifia sifia ni mbunge
mwenye msimamo ila nampongeza sana Waziri Lukuvi ni waziri mchapakazi
na kazi zake zinaonekana na ndio maana hata bungeni ni waziri pekee
ambaye bajeti yake ilipitishwa kwa kishindo hata na sisi wabunge wa
kambi ya upinzani”