UVCCM Wawabeza CCM.......Wadai Mzee Mwinyi Hakukosea Kutoa Maoni ya Rais Magufuli Kuongoza Milele
Ndugu Waandishi wa Habari
Kwa heshima kubwa tunawashukuru kwa dhati na kwa uungwana wenu wa kuitikia wito wetu wa kuwaomba kuhudhuria mkutano wetu huu ili kuzumgumza nanyi kama ilivyo ada na kawaida na hatimaye muweze kufikisha ujumbe wetu kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Ndugu Wandishi wa Habari
Itakumbukwa kuwa hivi karibuni katika moja ya Baraza la Idd El Fitri lililofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijijini Dar es Salam, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Mzee Ali Hassan Mwinyi, alitoa maoni yake binafsi baada ya kuutazama, kuudurusu na kuridhika na utendaji wa Serikali ya Awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk John Pombe Joseph Magufuli.
Ni ukweli usiofichika wala kupingika kuwa maoni ya Mzee Mwinyi bila shaka yoyote yatakuwa yamepata mshawasha baada ya kuvutiwa mno na uchapakazi wa Rais Magufuli, pia maoni hayo hayakuwa ni uamuzi wala shuruti kama ambavyo baadhi ya watu walivyokishilia bango na kulishupalia suala hilo kwa mtazamo hasi.
Maoni ya Mzee Mwinyi yalikuwa bayana au kwa lugha nyingine ni maoni mubashara yanayoweza kumlazimisha kila binadamu mwenye akili timamu afahamu kwa yakini alichotamka katika matamshi yake. Alichosema au kushauri ni jambo lenye mantiki kulingana na mtazamo wake ambao kwa hakika ulijiegemeza chini ya uhalisia wa mazingira ya nyakati na utendaji wa Rais Dk John Pombe Joseph Magufuli kwa kadri unavyoonekana.
Kwa bahati mbaya sana, eti wanaojiita ni wazee wa CHADEMA bila kufanya tafakuri, uchambuzi wa maana katika dhana kamili yenye uyakinifu wa jambo hilo, jana wakajikuta wakikurupuka, na kumuandama Rais Mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi bila ya kuwa na sababu za msingi kwa kumtolea maneno yasiyo na kichwa wala miguu.
Tokea Rais Dk John Pombe Magufuli aingie madarakani baada kuchaguliwa kidemokrasia na wananchi mwaka 2015, sasa yapata miaka miwili, utendaji wa Serikali yake ya awamu ya tano licha ya kumvutia kila mtanzania, umeitikisa na kuamsha mjadala nchini, Afrika Mashariki, Afrika na Dunia nzima .
Mjadala ni kuhusu kipimo cha utendaji wake unaochukua nafasi pana katika vichwa vya Magazeti ya nje na ndani, kwenye vipindi vya runinga na mitandao ya kijamii, Kitaifa na Kimataifa yote ikiwa ni katika kuutazama uadilifu wake, uwazi na uwajibikaji wa Serikali yake chini ya misingi ya uzalendo.
Watu mbalimbali wamekuwa wakijadili kutokana na kushawishika kwao Rais Magufuli kuhusu umakini alionao, uchungu kwa nchi yake na watu anaowaongoza akiwa na azma ya kupigania na kutetea maslahi ya umma huku akitaka rasilimali za nchi kuinufaisha nchi na watu.
Hakuna mtu au kiongozi wa ndani au nje ya chama tawala na nje ya nchi waliotumwa wajadili wanavyojadili iwe kwa kumpongeza na kumsifu kunakofanywa na watu hao.
*Ndugu Waandishi wa Habari*
Waswahili wa kale na wahenga wana semi mashuhuri isemayo“Kizuri hujiuuza na kibaya Hujitembeza”. Yaonekana ndivyo inavyotokea kwa walimwengu wanavyoutazama na kuufuatilia uongozi wa Awamu ya tano chini ya Rais Dk John Magufuli na Serikali yake katika mtazamo chanya wenye mafanikio.
Alichokisema Mzee Mwinyi si kuwataka au kuwashawishi wananchi kufanya mabadiliko ya Katiba hatimaye kumpa nafasi ya vipindi vingine vya utawala Rais John Magufuli abaki madarakani kinyume na matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Matamshi ya Mzee wetu Ali Hassan Mwinyi aliyaweka bayana akiyatanguliza utangulizi wa maneno adhimu na dibaji yaliosema nanukuulaiti nchi yetu isingelikuwa si yenye kufuata utawala wa kikatiba, Rais Dk John Magufuli alitosha na kufaa kuongoza nchi yetu kwa siku na miaka mingine.
Umoja wa Vijana ya CCM (UVCCM) hatuoni kama hilo ni kosa au baa, ama iwe mwao au uonekane uchuro kutokana na maneno hayo. Mzee Ali Hassan Mwinyi ni mweledi, mlinzi mzuri wa Demokrasia na mtu anaheshimu Katiba, Katu hakusema na kutaka Katiba ibadilishwe ili Rais abaki madarakani kama inavyopotoshwa kauli yake.
Ndugu Waandishi wa Habari
Hata hivyo inaonyesha wanaojiita Wazee wa CHADEMA hawana kumbukumbu ya kutosha. Wamesahau Rais wa Awamu ya Kwanza Baba wa Taifa marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitawala kwa kipindi cha miaka 23 tokea mwaka 1961 hadi mwaka 1985.
Mwalimu Nyerere hakutawala miaka 23 kwa lazima yake, nguvu za udikteta au kutumia misuli ya ubabe, alitawala kwa matakwa, ridhaa, utashi na maamuzi ya wana nchi wenyewe ndiyo waliomshinikiza na kumuomba kila wakati abaki madarakani kila alipopania kujiuzulu na kumpisha mtu mwingine.
Ifahakime kuwa Nchi yoyote na mahali popote, dunia inahitaji ipate mtawala na utawala wenye tija, manufaa na maendeleo yanayoonekana, kuwaridhisha au kuwapendezesha na kuwanufaisha wananchi.
Kushawishika na kuhamasika kwa wananchi na watu mbali mbali juu ya kazi nzuri inayofanywa na Dkt. Magufuli nadhani imewakumba mpaka Viongozi wenye nyadhifa mbali mbali katika Vyama Vya Siasa na makundi mengine. Mfano siku za karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la wananchi na wanachama wa Chadema wakiwemo madiwani sita kwa hiari na ridhaa yao wameamua kuachia ngazi na kukikimbia Chadema wakirejea CCM kwa kuridhika, kutosheka na utendaji wa Serikali ya Rais Dk John Magufuli.
Wanaojiita Wazee wa Chadema ingelipendeza sana kama wangekuwa na mapenzi na chama hicho wangalikaa chini kutafakari na kutathmini sababu ipi inayowafanya wanachama, viongozi waandamizi na madiwani hasa katika Mkoa wa Arusha wakikimbie chama hicho na kurejea CCM badala ya wazee hao kucheza ngoma isiowahusu.
Ndugu Waandishi wa habari
Wote hapa tunaelewa Katiba ya nchi si Quran wala Bibilia. Katiba imetungwa kutokana na maoni, weledi na utashi wa watu. Na watu hao hao kwa kujali kwao mahitaji na matakwa yao, wanaweza kugeuza chochote ndani ya katiba kwa kujali maslahi yao na wala isiwe baa au muujiza.
Umoja wa Vijana wa CCM unaamini ukishafikia hatua ya uzee wakati mwingine unapoteza kumbukumbu muhimu, tunawakumbusha wanaojiita wazee wa CHADEMA hakuna ushahidi unaoonyesha Mzee Mwinyi aliwahi kuwa na mpango wa kutaka kujiongezea muda ili abaki madarakani kama ilivyodaiwa na genge la Wazee hao. Kama mjuavyo kule Chadema kuna maprofesa wa kuzua hili nalo Mzee Mwinyi wamemzulia na kumpakazia.
Ingalikuwa Mzee Mwinyi alitamani kujiongezea muda ili aendelee kubaki madarakani kwa wakati ule, angeweza kwa sababu uongozi wake uliwakuna na kuwapendezesha mno wananchi mijini na vijijini na wala isingelikuwa ni kazi kubwa ya kukubalika na kuungwa mkono .
Zipo semi na hadithi nyingi zinazodai Mwalimu Nyerere katika Kitabu chake cha Tanzania na Hatma ya Uongozi alikiandika kwa lengo la kuwalenga viongozi aliowakusudia kuwapasha na kutaka wajisahihishe, kujisuta, kujiuzulu au kujirejebisha.
Ukweli ulivyo si hivyo, Mwalimu kama Mwalimu kitaaluma aliandikia Kitabu chake kwa msukumo wa maono yake ili kuiasa nchi yetu, viongozi wa sasa na wajao pia kuitazama hatma ya nchi yetu kiutawala, kidemokrasia na kiutendaji bila kumlenga au kumdhamiria yeyote kama inavyodaiwa na makuhani wa kuzua.
Ndugu zangu Waandishi wa habari.
Mtu mwerevu siku zote anapotaka kumuasa mwenzake atoe kibanzi katika jicho lake, kwanza huanza kutoa yeye boriti katika jicho lake. Kama tujuavyo Katiba za baadhi za vyama vya Siasa vikiwemo vile vya Ukawa. Katiba zao zinalalamikiwa kwa madai ya kuwa na udikteta.
Tumeshuhudia mivutano ikirindima ndani ya vyama hivyo huku viongozi wa Vyama hivyo wakigombana kwa sababu ya kulinda matakwa ya Katiba zao na baadhi yao wamekuwa ni zaidi ya wafalme na masultani waliojenga himaya ndani ya Vyama vyao huku wakiwa hawana ndoto wala fikara ya kuachia madaraka.
Wapo wanachama wengine wamefukuzwa na hata kuvuliwa uanachama ndani ya vyama vya upinzani kwasababu ya kutaka kuwania nyadhifa za juu ambazo wakubwa hawataki ziguswe kwakuwa kushika nafasi hizo ni kunagusa maslahi yao.
Wengine wanadaiwa kupoteza maisha katika mazingira ya kutatatanishi kwa kujaribu kwao kuchukua fomu za kuwania nafasi za juu huku wagombea urais wengine waliohama toka vyama vingine walipojiunga na vyama hivyo nyakati za asubuhi, jioni yake wakapitishwa kwa mbwembwe kuwa wagombea urais kinyume na matakwa ya Katiba zao .
Ndugu Waandishi wa Habari
Mwisho Umoja wa Vijana wa CCM tunawataka wazee maslahi wa Chadema waache kulishwa maneno na kuwa wazushi na waongo, waache papara ya kujibu kila wanachokisikia kwa kuchochewa na ushabiki baada ya kuoayiwa milungula na bahashish na kukimbilia kuwadhalilisha viongozi waliolitumikia Taifa hili kwa uadilifu na bidii na juhudi huku wakiongoza nchi kwa hekima, busara kubwa zilizosaidia kuleta mageuzi kadhaa ya kiuchumi, kijamii na kisiasa yalioacha alama ya utumishi wao uliotukuka kwa watanzania.
Tunaendelea kuwaaminisha watanzania Chama Cha Mpainduzi ni chama kikubwa ndani Afrika na duniani kwa ujumla hivyo siku zote hakifanyi makosa katika kuwaletea viongozi makini, wenye upeo na uweledi wa hali ya juu.
Ahsanteni
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Shaka Hamdu Shaka (MNEC)