TRL Yavikataa vichwa vya treni Vilivyo Bandarini.......TPA Wanadai ni Vyao ila tu Kuna Mgogoro Ambao wao Hawakutaarifiwa
Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) imekanusha kuhusika na vichwa 11 vilivyoshushwa na kutelekezwa katika Bandari ya Dar es Salaam hivi karibuni.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko, vichwa hivyo vilivyoshushwa na meli ya Mesina Line tangu wiki iliyopita, na kwamba ni mali ya TRL.
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Masanja Kadogosa jana alisema TRL haihusiki kwa namna yoyote na vichwa hivyo kwa kuwa hakuna taarifa zozote zinahusu uagizwaji wake.
Alisema pia kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi, kampuni hiyo inapofanya manunuzi yoyote lazima kuwepo na mkataba wa makubaliano na kampuni husika inayouza bidhaa, lakini haina mkataba wowote unaohusu ununuzi wa vichwa hivyo.
Alieleza kuwa taratibu za manunuzi zinafahamika kwani endapo kampuni hiyo ingeagiza vichwa hivyo ingetakiwa kupeleka mtu wake kwa ajili ya ukaguzi wakati vinatengenezwa na mara baada ya kutengenezwa kabla ya kupakiwa kwenye meli. “Lakini hiyo kitu hakuna, hatukuwa na watu wetu kwa kuwa si mali yetu,” alieleza.
Pamoja na hayo, alisema ili mzigo wowote umfikie mhusika lazima kuwepo na nyaraka ya kutolea mzigo bandarini ambayo pia huwa na makubaliano mengine baina ya mnunuzi na muuzaji ambayo katika sakata hilo, TRL wamesisitiza hawana nyaraka hiyo.
Alisema TRL haivitambui vichwa hivyo kwa kuwa si mali yake. “Hivi ni vichwa vikubwa sasa kwanini tuvikatae kama ni vyetu, ila ukweli ni kwamba hatuvitambui kabisa,” alieleza mkuu huyo wa reli nchini.
Juzi wakati akizundua Mradi wa Uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam (DSMGP), Rais John Magufuli aliibua hoja hiyo ya vichwa vya treni kushushwa bandarini na kutekelezwa bila kuwa na mwenyewe na kuitaka TPA pamoja na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, kufuatilia kwa kina suala hilo.
Dk Magufuli alisema anazo taarifa za kushushwa kwa vichwa vya treni takribani 15 katika bandari hiyo, ambavyo mmiliki wake hafahamiki na meli iliyovileta imeshaondoka.
Hata hivyo, mkurugenzi wa mamlaka hiyo ya TPA Kakoko pamoja na kuthibitisha kushushwa kwa vichwa hivyo kutoka kwa meli ya Mesina Line, iliyobeba mzigo huo kutoka kwa Komazi Trading Co, alibainisha wazi kuwa vichwa hivyo ni vya TRL.
Alisema vichwa hivyo ni awamu ya pili iliyoagizwa tangu serikali ya awamu ya nne miaka mitatu iliyopita, ambapo awamu ya kwanza ilishaletwa na vichwa vyake kuchukuliwa na hadi leo vinatumiwa na TRL.
Alifafanua kuwa baada ya uchunguzi wa TPA ilibaini kuwa kuna mgogoro unaoendelea kati ya TRL na kampuni ya Komazi na kwamba TRL ilishagoma kuvichukua vichwa hivyo lakini suala hilo, halikutaarifiwa kwa TPA