SERIKALI YAMWAGA AJIRA 10,184 KUZIBA NAFASI ZA WATUMISHI WENYE VYETI FEKI


OFISI ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imetangaza kutoa vibali vya ajira 10,184 ili kuziba nafasi zilizoachwa wazi na watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti vya elimu, imefahamika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Rais, Utumishi, Florence Temba, ilieleza kuwa agizo hilo linazihusu Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sekretarieti za Mikoa, Wakala wa Serikali, pamoja na Taasisi na Mashirika ya Umma.

Ilimnukuu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki akitoa agizo hilo wakati akizungumza katika kikao kazi na watumishi wa Umma wa Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam jana.

“Mgawanyo wa vibali vya ajira umezingatia upungufu uliojitokeza baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki, vipaumbele vya Taifa kwa sasa na upatikanaji wa watumishi kutoka katika soko la ajira,” alisema Kairuki.

Kairuki aliongeza kuwa taratibu za kukamilisha mgawo wa nafasi za ajira 4,816 zilizosalia unaendelea ili kuwezesha wizara na taasisi nyingine zilizokamilisha uhakiki wa watumishi wa umma hivi karibuni kuajiri watumishi wapya kuziba nafasi wazi zilizojitokeza.

Alieleza kuwa serikali imetoa kibali kuajiri watumishi wapya 15,000 ili kuziba pengo lililosababishwa na kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti baada ya zoezi la uhakiki.

“Watumishi wa umma watakaoajiriwa kuziba nafasi hizo wanatarajiwa kuripoti kazini kuanzia mwezi Agosti, 2017,” alieleza Waziri Kairuki, na kuongeza kuwa utaratibu wa ajira mpya za serikali upo palepale na amewataka wananchi kutokuwa na wasiwasi wowote wa ajira hizo.

“Napenda kusisitiza kuwa vibali tulivyovitoa leo ni vile vilivyoziba pengo la walioghushi vyeti, naomba wananchi watambue kuwa suala la ajira mpya bado liko pale pale kama serikali ilivyojipanga,” alisema Kairuki.

Aprili mwaka huu, Rais John Magufuli alipokea ripoti yenye orodha ya watumishi wa umma ambao kati yao wanadaiwa kuwa na vyeti pungufu, vyenye utata na vya kughushi kutokea kwa Waziri Kairuki.

Waliokuwa na vyeti vya kughushi walikuwa 9,932, na Rais aliapa kwamba hawatarudi kazini. Rais Magufuli aliagiza kufutwa kazi kwa wote waliotajwa kwenye ripoti hiyo na kuzuia mishahara yao ya mwezi huo, lakini hata hivyo bado mlango uliwekwa wazi kwa wenye pingamizi na wapo waliokataa rufaa huku wengine wakienda kwenye mamlaka husika kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.

Wiki iliyopita akiwa Dodoma, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro alitangaza kuwa wiki hii serikali itatoa vibali 3,000 vya ajira katika sekta ya afya vikiwemo vya madaktari na wauguzi pamoja na maofisa hesabu 535 kwa ajili ya vituo vya afya vya kata ili washughulike na ukusanyaji wa mapato kwenye vituo vya afya na zahanati.
Chanzo-Habarileo
Powered by Blogger.