Serikali Kuunda Kamati ya Kukagua Viwanda Vyote Nchini
Serikali
imeteua kamati maalumu yenye kushirikisha wataalamu pamoja na wakuu wa
mikoa wa kila mkoa, itakayozunguka kukagua utendaji wa viwanda
vilivyobinafsishwa, na kisha ndani ya siku 15 itatoa maamuzi.
Imesema
viwanda watakavyoshughulika navyo ni vile vilivyobinafsishwa na ambavyo
havifanyi kazi, lakini pia kuhakikisha uzalishaji wa kiwanda husika
kama ndio ulioruhusiwa.
Waziri
wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema hayo jijini
Dar es Salaam jana na kuongeza kuwa wapo waliopewa viwanda kwa shilingi
moja na wengine kwa Sh milioni 10, vingine vikifanya kazi, vingine
vikiwa havifanyi kazi iliyokusudiwa na vingine kutokufanya kazi kabisa.
Alisema
Kamati hiyo itafuatilia na tayari ameandika barua kwa wakuu wote wa
mikoa nchini, na kupewa hadidu za rejea ili waweze kupitia kiwanda
kimojakimoja kuhakikisha utendaji kazi wake.
“Wakati
Kamati hiyo ikikagua, wakikiona kiwanda wanapiga simu kwake na kwa
msajili wa hazina ili kwenda kuhakikisha kiwanda hicho kinafanya kazi na
baada ya hapo Augusti 15 watafanya maamuzi,” alisema.
Alisema
yeyote aliyepewa kiwanda ni lazima kifanye kazi na kwamba kama
anayehusika ameshindwa, atafute mtu mwingine ili kifanye kazi, la hasha
ameagizwa akakichukue, kwani wapo watanzania ambao ni vijana wanatafuta
kazi wakihitaji kutolewa vijiweni na kupewa viwanda waviendeshe na
taasisi za kuwaelekeza zipo.
Alisema
lengo la kubinafsisha viwanda ni ili vizalishe bidhaa ambazo zitatumika
nchini na nyingine ziweze kuuzwa nje ya nchi na kuleta fedha za kigeni,
vifanye kazi viweze kutoa ajira kwani asilimia 65 ya idadi ya watu
nchini n I vijana na wengi wao hawana ajira.
“Kuna
viwanda vilivyobinafsishwa na vinafanya kazi, hivyo hatuna shida navyo
bali vile ambavyo havifanyi kazi, kwani malengo yetu ni wote wenye
viwanda vifaye kazi hata vile vilivyosimama ili vikidhi malengo
yaliyotakiwa,” alisema Mwijage na kuongeza kuwa viwanda vingi vilitolewa kwa Shilingi moja na vingine hadi Shilingi milioni 10.
Alitoa
wito kwa wakuu wa mikoa, kukagua kiwanda kimoja baada ya kingine na
hata kuhoji umiliki, hivyo mhusika anatakiwa kuwa na nyaraka stahiki,
kwani ubinafsishaji dhamira yake kubwa ilikuwa ni kuwepo kwa ajira.