Rufaa Vyeti Feki: 600 Wagonga Mwamba, 450 Warudishwa Kazini
Watumishi
wa umma 450 walioondolewa kazini kutokana na kudaiwa kutumia vyeti vya
kughushi wamerudishwa kazini baada ya kushinda rufaa zao.
Baada ya kutangazwa kwa Orodha ya watumishi wenye vyeti feki, 1050 walikata Rufaa huku 8800 wakiridhika na matokeo hayo.
Mbali
na hilo, Serikali imesitisha mishahara kwa watumishi wa umma ambao
walitakiwa kuwasilisha vyeti vyao kwa uhakiki lakini mpaka sasa
hawajafanya hivyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk.Laurean
Ndumbalo alisema watumishi hao wameshinda rufaa zao hivyo wataandikiwa
barua za kurudishwa katika utumishi wa umma.
Alisema katika rufaa hizo, wengi walikuwa wanawake walioolewa na kubadili majina yao kwa kutumia ya waume zao.
“Kuna
baadhi walitumia majina mawili alipokuwa kidato cha nne baadaye
alilazimika kutumia matatu na kusababisha mkanganyiko hivyo
tumejiridhisha na wanarudishwa katika utumishi wa umma,” alisema Dk. Ndumbalo.
Alisema
Serikali pia imesitisha mishahara kwa watumishi wa umma ambao
walitakiwa kuwasilisha vyeti vyao kwa uhakiki lakini mpaka sasa
hawajafanya hivyo.
“Serikali
imesitisha mishahara ya watumishi wote ambao muundo wa utumishi wao
uliwataka kuwa na sifa ya kufaulu kidato cha nne wakati wanaajiriwa
lakini hawakuwasilisha vyeti vyao kuhakikiwa na Baraza la Mitihani.
“Tunasitisha mishahara yao kuanzia mwezi Julai hadi hapo watakapowasilisha vyeti vyao kuhakikiwa,” alisema Dk. Ndumbalo.
Dk.
Ndumbalo aliongeza kuwa kwa watumishi walioajiriwa wakiwa darasa la
saba kabla ya waraka wa Utumishi wa Umma namba moja wa mwaka 2004
uliowataka waajiriwa kuwa na sifa ya kidato cha nne, wataendelea na kazi
mpaka watakapostaafu.
Alisema
sera ya Menejimenti na Ajira katika utumishi wa umma toleo la mwaka
1998 lilianza kutekelezwa Mei 20, 2004 hivyo kwa walioajiriwa kabla ya
hapo warudishwe kazini kama waliondolewa kimakosa.
“Nasisitiza
kuwa watumishi wote wa umma walioajiriwa kwa sifa ya elimu ya darasa la
saba kabla ya Mei 20 hawahusiki na uhakiki wa vyeti vya kufaulu mtihani
wa kidato cha nne na wataendelea kuwa watumishi wa umma katika vyeo
vyao mpaka watakapostaafu kazi,” alisema Dk.Ndumbalo.