Rais Magufuli Kuzindua Mradi Mkubwa wa Maji Sengerema Kesho
Rais John Magufuli anazindua mradi mkubwa wa maji katika kijiji cha Nyamazugo wilayani Sengerema kesho.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole alisema jana kuwa, Rais Magufuli atafika wilayani hapo saa mbili kwa ajili ya uzinduzi huo.
Mradi huo ulioanza kutekelezwa tangu mwaka 2014 kwa gharama ya Sh23 bilioni utawanufaisha zaidi ya wakazi wa wilaya hiyo zaidi ya 13,000.
“Lakini akiwa njiani kuelekea katika tukio la kuzindua mradi huo atasalimiana na wananchi barabarani kadri itakavyowezekana na baada ya kuzindua mradi huo atawahutubia wananchi wa Sengerema na viunga vyake hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi,” alisema Kipole.
Kipole alisema wilaya hiyo ina jumla ya wakazi 74,186 kutokana na Sensa ya Watu na makazi ya mwaka 2002, hivyo mradi huo kwa sasa utahudumia kata 11.
Kata hizo ni Sima, Nyatukala, Ibisabageni, Mwabaruhi, Nyampulukano, Misheni, Tabaruka, Nyampande, Nyamazugu, Nyamazeze na Ibondo.
Mhandisi wa Maji Wilaya ya Sengerema, Nikas Ligombi alisema mradi huo uliofadhiliwa na Benki ya Afrika umekamilika kwa asilima 100 na utakapozinduliwa rasmi tatizo la maji katika mji wa Sengerema litakuwa limepatiwa ufumbuzi.
“Lita za ujazo 150,000 zitakuwa zinasukumwa kila siku kutoka kwenye chanzo cha maji kwenda kwenye matanki ya kusambaza mitaani,” alisema Ligombi.
Mkuregenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Sengerema, Magesa Mafuru alisema ni fahari kubwa kukamlika kwa maradi huu ambao utamaliza matatizo ya maji yaliyokuwa yakiukabili mji huo na kuwataka wananchi kuutunza na kuuthamini ili udumu kwa muda mrefu.
Mmoja wa wakazi wa mjini humo, Jumanne Kashiba alisema baada ya mradi huu kukamilika tatizo la maji mjini hapo lilokuwa likiwakabili litakoma na kuipongeza serikali kwa jitihada hizo.