Rais Magufuli Amvaa Tundu Lissu.....Awataka Watu wa Singida Wasirudie Kosa 2020
Rais
Magufuli, amesema kuwa suala la maendeleo halina itikadi kwani
yanayofanywa na Serikali yake hata mtoto wa Mbunge wa Singida Mashariki,
Tundu Lissu (Chadema) atanufaika nayo.
Kutokana hali hiyo alisema bado ataendelea kuwafanyia kazi Watanzania, huku akipambana na watu wanaohujumu rasilimali za Taifa.
Kauli
hiyo aliitoa jana mjini Itigi Manyoni mkoani Singida, ambapo alisema
hatobagua vyama ila kwa sasa Tanzania inahitaji maendeleo ya kweli na si
maneno.
Kiongozi
huyo wa nchi alisema anashangazwa na baadhi ya watu kupiga kelele
wakiwa jijini Dar es Salaam wakati majimbo yao hayana watu wa kuwasemea
kwa kukosa maji, umeme na huduma za afya.
“Ukiona
makelele yanapigwa ujue ni rushwa waliyopewa na hao watu..kama ni
mmoja, wawili watatu ninawaambia wawekeni kiporo ili muwamwage katika
uchaguzi ujao.
“Maendeleo
ni ya wote awe mtoto wa nani au mtoto wa nani hata mtoto wa Tundu
Lissu. Mna matatizo mengi mahosipitali na mengine lakini hamna wa
kuwasemea badala yake wanazungumzia ya Dar es Salaam. Acha mkome si
mlichagua wenyewe!
“Kosea
njia usikikosee kuoa mke, usije pia kukosea kuchagua na kukosea madhara
yake ni makubwa. Mwaka 2020 ikifika msikosee tena,” alisema Rais Magufuli.
Pamoja na hali hiyo alisema kama kuna tochi inawaka basi ina betri “Ukiona mtu anapiga kelele ujue kuna kitu amemeza na sio kingine bali ni rushwa, ukiona tochi inawaka ujue kuna betri,” alisema.
Alisema
kuhusu ujenzi wa barabara hiyo itatumia na watu wote wakiwemo wanachama
wa Chadema, ACT-Wazalendo jambo ambalo siku zote husimamia dhana
maendeleo hayana chama.
Alisema
ndani ya Serikali kuliwa na watu watumbuaji kwa kuwa na safari kila
kukicha ikiwemo kufanya semina kila mahali ikiwemo nchi za Ulaya huku
Watanzania wakiendelea kuumia kwa kukosa maendeleo.
“Nimeamua
kuanza na watu wa juu na ninawatumbua kweli kweli kazi ni ngumu unaweza
kutumbua ukakutana na usaha ukakurukia kwenye macho.
“Niombeeni nitumbue salama nisije kutumbua watu ambao hawatakiwi kutumbuliwa,” alisema.
