Rais Magufuli amuweka njia panda Chiza


Rais John Magufuli ameshangazwa na kauli ya Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo na Biashara nchini Christopher Chiza kuwa na mipango ya kujenga majengo mapya kwa ajili ya wafanyabiashara badala ya viwanda vitakasaidia nchi.

Akizungumza leo wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya 41 ya Biashara ya Kimataifa, Rais Magufuli amesema kwamba ameshangazwa sana na mipangio ya kujenga mahoteli pamoja na kufanyia ukarabati wa majengo kwani hajui mahali pesa hizo zitakapopatikana.

"Mh. Chiza amezungumza kubadilisha majengo na kujenga mapya, mawazo mazuri lakini najiuliza hizo hela zimetoka wapi , haingii akilini wao ndio wanatusisitizia mambo ya biashara na viwanda na 'theme' ya mwaka huu inazungumzia kukuza biashara na maendeleo ya viwanda sasa wao badala ya kuzungumza juu ya maendeleo ya viwanda wanataka wajenge Hotel hapa, watengeneze majengo mapya sasa. Sijaelewa, sasa kama hizo hela zipo basi mzipeleke mkajenge kiwanda cha mfano

Aidha Rais magufuli amesisitiza kwamba "Haya majengo yaliyopo ambayo mnayaona yamechakaa hawa wanaokuja kuonesha bidhaa zao wapeni bure wajenge ili kila mwaka wawe wanaonesha, hiyo Hoteli kwani mkijenga lazima walale hapa hapa? Mnaweza kujenga hoteli hapa bado wakaenda mjini. Mimi nilifikiri badala ya kujenga jenga majengo fikirieni zaidi katika kujenga viwanda kwa ajili ya mfano wa kuonesha Wizara kweli iko mbele kwa ujenzi wa viwanda.

Katika kuonyesha nia ya kufikia Tanzania ya viwanda inafikiwa Rais ameitaka wizara pamoja na bodi hiyo kutofikiria ujenzi wa majengo.

"Mwenyekiti nimekuteua juzi umeshaanza kufikiria majengo hapa pamoja na Bodi yako mnanifanya nifikirie zaidi. Haya majumba yanaweza yakawa siyo mazuri sana lakini ni mazuri kwa watu wa Tanzania ambao wanataka kuona bidhaa. Yanayowaleta hapa siyo majumba Watanzania wanakuja hapa kuangalia Teknolojia na vifaa vilivyomo.Inawezekana mimi nipo tofauti mnisamahee lakini katika muelekeo wangu ninaona hizo hela mnataka kuzitumia vibaya" Rais alisisitiza.

Pamoja na hayo Mh. Rais amewaomba waandaji wa maonyesho hayo pamoja na Waziri wa viwanda na biashara Mh. Charles Mwijage kuongeza siku zaidi katika maonesho ili watanzania waweze kupata muda mzuri wa kununua na wafanyabiasha kuuza ambapo ombi lake lilikubaliwa hapo hapo na kuongezwa siku tano mbele.
Powered by Blogger.