Ndugai Aula....Achaguliwa Kushika Wadhifa Mzito Afrika
Ofisi ya Bunge inapenda kuuarifu umma kuwa Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai (Mb), amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Maspika na Viongozi wa Bunge katika Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Barani Afrika.
Uchaguzi huo umefanyika katika Mkutano wa Maspika wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Barani Afrika uliomalizika jana Mjini Abuja.
Kwa
wadhifa huo, Mhe Ndugai ataongoza Maspika wenzake toka Mabunge na
Mabaraza ya kutunga Sheria 63 yaliyoko katika nchi 18 za Jumuiya ya
Madola kwenye Bara la Afrika.
Wadhifa huo ni wa miaka miwili kuanzia sasa hadi mwaka 2019 kutakapofanyika uchaguzi mwingine.
Nchi
wanachama wa Umoja wa Mabunge Barani Afrika ni pamoja na Afrika ya
Kusini, Botwana, Cameroon ,Ghana, Kenya, Lesotho, Msumbiji, Mauritius,
Malawi, Nigeria, Namibia, Rwanda, Seychelles, Sierra Leone, Swaziland,
Tanzania, Uganda na Zambia.
Akizungumzia uchaguzi huo, Mhe Ndugai amesema "Kwa
hakika nawashukuru Maspika wenzangu kwa kunipa dhamana hii ya kuwa
Mwenyekiti wao, ni heshima kwangu binafsi lakini zaidi Kwa Tanzania. Ni
matumaini yangu kwamba Bunge letu litaendelea kung'ara kitaifa na
kimataifa tukiwa Bunge moja lenye Upendo na mshikamano".
Huu
ni wadhifa wa nne kwa Mhe. Ndugai katika masuala ya Bunge kwenye medani
ya Kimataifa. Amewahi kuwa Mwakilishi wa Nchi za Afrika Mashariki
katika Kamati ya Utendaji ya Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola
Duniani mwaka 2008-2011, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii ya
Umoja wa Mabunge ya Afrika, Pacific na Carribbean na Jumuiya ya Ulaya
mwaka 2011-2014 na Rais wa Baraza la Mabunge ya Nchi za Kusini mwa
Afrika (SADC – PF)
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano
Ofisi ya Bunge
DODOMA