MWENYEKITI KAMATI YA UCHAGUZI TFF ALIVYOZUIA ZOEZI LA KUMPITISHIA MALINZI "MLANGO WA UANI"
KUULI (KATIKATI) AKIWA NA BAADHI YA WAJUMBE WA KAMATI HIYO YA UCHAGUZI.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Revocatus Kuuli ameonyesha msimamo wake na kusema asingeweza kukubali mambo ya upindishwaji ili kutoa ruhusa kwa baadhi ya wagombea kufanya usaili wa maandishi.
Kuuli ambaye ni wakili, amesema alipishana na wajumbe wa kamati hiyo wakiwa kikaoni wakitaka Jamal Malinzi na Geofrey Nyange 'Kaburu' wapewe nafasi ya kufanyiwa usaili kwa maandishi.
"Nisingeweza kuingia kwenye upindishaji wa mambo namna hiyo, siwezi kukubali na msomi yoyote wa kiwango changu asingekubali kufanya jambo kama hilo.
"Hivyo nimesisitiza utaratibu utakwenda kama ulivyopangwa, waliofika tumewafanyia usaili na mambo yamekamilika. Hivyo Jumapili (Leo) majina yao yatawekwa kuonyesha hao ndiyo wahusika," alisema.
Wajumbe walio kwenye kamati hiyo walionyesha wakitaka lazima Malinzi afanyiwe usaili licha ya kwamba yuko mahabusu ambako anakabiliwa na makosa kadhaa likiwemo la matumizi mabaya ya fedha na utakatishaji fedha.