MCHAPALO WA MIAKA 50 YA BENKI YA NBC WAFANA JIJINI MWANZA
Jana Julai 28,2017 usiku wa kuamkia leo jumamosi, mchapalo (sherehe) wa kusherehekea miaka 50 tangu kuanzishwa kwa benki inayolitumikia Taifa la Wachapakazi, NBC umefana Jijini Mwanza ambapo benki hiyo imekutana na wadau wake wakiwemo wafanyabiashara.
Kaimu Mkurugenzi wa benki ya NBC, Theobald Sabi alisema maadhimisho hayo yamefanyika Jijini Mwanza ikizingatiwa kwamba Jiji hilo ni la pili kwa ukubwa nchini na kwamba inao wateja wa muda mrefu wanaohudumiwa kwenye matawi yake matatu hivyo ni jambo jema kujumuika nao pamoja.
“Hakika NBC ina historia ndefu katika kujenga uchumi wa nchini yetu, ni jambo lisilopingika kwamba NBC ni mama wa benki za kibiashara hapa Tanzania”. Alidokeza Sabi huku akiwashukuru wafanyakazi wa benki hiyo waliojawa uzalendo, umakini na ubunifu katika kazi.
Mkurugenzi wa Bodi ya NBC, Dr.Kassim Hussein alisema moja ya hatua za benki hiyo ni kuwa kitovu cha malipo yote nchini (National Payment System) mfumo ambao hadi sasa unategemewa nchini. Alidokeza kwamba miaka ya 70 mbali ya kutoa huduma nchini nzima, vile vile benki hiyo ilikuwa ikitoa huduma kwa njia ya mawakala, ikawa mwanzishi wa mobile banking pamoja na huduma za bima.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Merry Tesha aliipongeza benki ya NBC kutokana na mapinduzi yake kwenye sekta ya kifedha nchini na kuiomba kuwekeza moja kwa moja ama kwa ubia katika utekelezaji wa azima ya serikali ya ujenzi wa viwanda nchini ikiwemo kutoa mikopo kwa wawekezaji wa ndani.