Hotuba Ya Waziri Mkuu Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania, Wakati Wa Kuahirisha Mkutano Wa Saba Wa Bunge La Kumi Na Moja Tarehe 05 Julai, 2017
UTANGULIZI:
1.
Mheshimiwa Spika, leo tumefika mwisho wa Mkutano wa Saba wa Bunge la 11
ulioanza Jumanne ya tarehe 4 Aprili, 2017. Tunayo kila sababu ya
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuifikia siku hii, tena baada
ya kuwa tumetimiza wajibu wetu wa Kikatiba kikamilifu na kwa umahiri
mkubwa.
Huu
ulikuwa ni Mkutano muhimu sana kwa nchi yetu kutokana na jukumu kubwa
la kujadili na kupitisha bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
ulioanza tangu tarehe 1 Julai, 2017. Bajeti hii ambayo ni nzuri na ya
kihistoria ni ya pili tu kati ya takribani Bajeti tano za Serikali ya
Awamu ya Tano zitakazoandaliwa hadi kifikia Mwaka wa Fedha 2020/2021.
2.
Mheshimiwa Spika, wakati Bunge lako likiendelea, tarehe 13 Aprili, 2017
tulipokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya askari
polisi wetu 8 waliopoteza maisha wakiwa wanalitumikia Taifa kwa kuuawa
na kundi la wahalifu katika eneo la Jaribu Mpakani, Wilayani Kibiti
mkoani Pwani. Askari hao waliopoteza maisha ni Inspekta Msaidizi Peter
Kiguu, Koplo Francis, PC Haruna, PC Jackson, PC Zakaria, PC Siwale, PC
Maswi na PC Ayoub. Pia, hivi karibuni mwezi Juni, 2017 Askari wetu
wawili wa Kikosi cha Usalama Barabarani walivamiwa na kupigwa risasi na
majambazi katika Kijiji cha Bungu “B” kilichopo Wilayani Kibiti. Aidha,
wananchi wetu wengi wamepoteza maisha kutokana na uhalifu unaofanywa na
majambazi waliopo katika maeneo ya Kibiti, Rufiji na Mkuranga.
3.
Mheshimiwa Spika, natumia fursa hii kulaani kitendo hicho cha kihalifu,
na kutoa pole kwa Inspekta Jenerali wa Polisi kwa kuondokewa na vijana
hao shupavu. Aidha, natoa pole kwa familia za wafiwa wote kwa kuondokewa
na wapendwa wao. Mauaji ya Wananchi wetu na askari wetu hayakubaliki na
wala hayavumiliki, kwani Askari ndio walinzi wetu sisi pamoja na mali
zetu. Aidha, tishio kwa walinzi wa amani na wananchi wetu ni tishio
kwetu sote, hivyo, Serikali itahakikisha waliohusika na mauaji hayo
wanakamatwa na kuchukuliwa hatua stahiki. Wanaweza kukimbia, lakini
hawataweza kujificha daima. Tutawakamata!.
4.
Mheshimiwa Spika, asubuhi ya tarehe 6 Mei, 2017, nchi yetu iliamka na
simanzi kubwa kufuatia ajali iliyogharimu maisha ya watu 36, wakiwemo
wanafunzi 33, walimu wawili na dereva wao, waliokuwa kwenye safari ya
kimasomo Wilayani Karatu. Ajali hiyo imezima ndoto za vijana hao na
kuacha vilio kwenye familia zao. Namuomba Mwenyezi Mungu azilaze mahali
pema Peponi roho za marehemu. Aidha, nawaomba wazazi, walezi, walimu na
marafiki wa watoto hao waendelee kumtumainia Mwenyezi Mungu kwa mtihani
huo mkubwa walioupata. Naendelea kutoa wito kwa vyombo vyote
vinavyohusika na ukaguzi wa vyombo vya moto vya usafiri kwa wanafunzi na
abiria wafanye ukaguzi wa kina na wa mara kwa mara ili kuliepusha Taifa
na ajali zinazoweza kuzuilika.
5.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu pia ilipata pigo la kuondokewa na watumishi
wawili wastaafu waliolitumikia Taifa hili kwa umahiri na uadilifu
mkubwa. Watumishi hao ni marehemu Paul Sozigwa, aliyekuwa Katibu wa Rais
wa Awamu ya Kwanza; na Marehemu Said Mwambungu, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa
wa Ruvuma. Namwomba Mwenyezi Mungu awape pumziko la amani marehemu wote
baada ya kulitumikia Taifa letu kwa utumishi uliotukuka na umahiri
mkubwa.
SHUGHULI ZA BUNGE
6.
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, Bunge lako Tukufu limejadili na
kupitisha bajeti za Wizara zote 19 na Bajeti nzima ya Serikali Kuu,
kupitisha Maazimio matano (5) ya kuridhia Mikataba mbalimbali ya
Kimataifa na kupitisha Miswada ya Sheria mbalimbali, ambayo ni Muswada
wa Sheria ya Fedha za Matumizi; Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka,
2017; Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka
2017; Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi
katika Mikataba inayohusu Maliasili za Nchi, 2017; na Muswada wa Sheria
ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili.
7.
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu jumla ya maswali 499 ya msingi na
mengine 1,834 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa
na Serikali kupitia kwa Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na maswali
ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu. Vilevile, katika kipindi hiki Ofisi ya
Bunge iliendesha Semina mbalimbali kwa Waheshimiwa Wabunge kwa lengo la
kuwajengea uwezo zaidi na kuwapa uelewa mpana wa masuala mbalimbali
yanayohusu maendeleo ya nchi yetu.
8.
Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu pia lilipata fursa ya kuchagua
Wawakilishi wa Tanzania kwenye Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki,
ambapo Wabunge tisa walichaguliwa. Kati ya Wabunge hao, watano ni
wanawake, na wanne ni wanaume. Ni matumaini yangu kuwa Waheshimiwa
Wabunge hao wataiwakilisha vema nchi yetu na kwamba watatimiza
kikamilifu wajibu wao kwa mujibu wa Mkataba wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
inaelekezwa kufanya kazi kwa karibu na Wabunge hao ikiwa ni pamoja na
kuwapa ushirikiano unaostahili ili waweze kutekeleza vizuri majukumu yao
kwenye Bunge hilo.
9.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kukushukuru wewe binafsi Mheshimiwa
Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali na timu yake, Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri,
Waheshimiwa Wabunge na Watendaji na Wataalam wa Serikali pamoja na
watumishi wa Ofisi ya Bunge kwa kufanikisha kazi zote zilizopangwa
kwenye Mkutano huu tena kwa ufanisi mkubwa.
10.
Ninawapongeza pia na kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri
kwa maelezo mazuri ya ufafanuzi waliyotoa wakati wa kujibu maswali
mengi ya msingi na ya nyongeza ya Waheshimiwa Wabunge pamoja na kujibu
hoja za Kamati za Kudumu za Bunge na hoja zilizotolewa na Waheshimiwa
Wabunge binafsi ndani ya Bunge zima. Serikali inathamini sana maoni na
ushauri wa Waheshimiwa Wabunge, na tunaahidi kuendelea kuzingatia maoni
na ushauri wao.