DC SHINYANGA APIGA MARUFUKU WAGONJWA KUOMBWA FEDHA ZA MAFUTA YA GARI
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro - Picha kwa hisani ya Malunde1 blog
MKUU wa Wilaya ya Shinyanga, Josephine
Matiro (pichani) amesema ni marufuku kwa wagonjwa kuombwa fedha za
kununulia mafuta ya gari ili wapate huduma ya kusafi rishwa kwenda
kupata rufaa hospitali kubwa wakati halmashauri imekwisha tenga bajeti
kwa ajili ya mafuta.
Matiro aliyasema hayo mwishoni mwa wiki
wakati alipokabidhiwa gari la kubebea wagonjwa na Mbunge wa Viti
Maalumu, Lucy Mayenga katika Kituo cha Afya cha Kambarage kinachohudumia
zaidi ya watu 28,500. Alisema ni marufuku mgonjwa kuombwa fedha kwa
ajili ya mafuta kwenye gari ili kupelekwa hospitali kupata rufaa kwani
halmashauri imetenga fedha za mafuta na hilo kama la uongo, alimtaka
mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo alithibitishe mbele ya wananchi.
Akizungumzia uhaba wa dawa alisema
tatizo hilo limekwisha patiwa ufumbuzi mpaka sasa anachokifahamu hakuna
tatizo hilo tena kwani serikali imekwishalifanyia kazi na malalamiko
madogo madogo yaliyokuwa yakitolewa na wananchi yamekwisha malizwa.
Naye mbunge Mayenga alisema ni bahati
kupata gari hilo kwani nchini kuna vituo vingi vya afya, hvyo ni jambo
la kushukuru kwani wasingeweza kununua gari hilo kwa haraka lenye
thamani ya zaidi ya Sh milioni 290 ikiwa bado kuna changamoto ya ukosefu
wa chumba cha upasuaji.
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya
Wilaya ya Shinyanga, Laurent Mhembe alisema kituo hicho kilianzishwa
mwaka 2010, na kimekuwa na ongezeko la wagonjwa mwaka 2014 baada ya
hospitali ya rufaa ya mkoa kupandishwa hadhi na kuwa kituo chenye
utegemezi mkubwa.IMEANDIKWA NA KARENY MASASY,- habarileo SHINYANGA