BAKWATA wataka anayejiitwa Mtume akamatwe

Baraza la ulamaa limetoa wito kwa vyombo vya dola kumchukulia hatua stahiki mtu aliyejitokeza katika Mkoa wa Pwani na kudai yeye ni Mtume.

Akizungumza  jana na waandishi wa habari kwa niaba ya Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir Ally,  Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu Bakwata, Sheikh Hamisi Said Mataka alisema, anachodai mtu  huyo anayefahamika kwa jina la Hamza Issa kuwa yeye ni Mtume  ni kitu ambacho hakipo kabisa katika mafundisho ya kiislamu.

Alisema kauli ya Issa kudai yeye ni mtume na kisha  kwamba ni muislamu na kutumia maandiko ya uislamu ni upotoshaji mkubwa ambao ukiachwa bila kudhibitiwa ni kuruhusu fujo na uvunjifu wa amani.

“Kwa mujibu wa maelezo yaliyoenea katika mitandao ya kijamii na ya kutoka baraza za Masheikh wa Mkoa wa Pwani chini ya kiongozi wake Sheikh na Qadhi wa Mkoa wa Pwani, amedai kuwa yeye ni Nabii Ilyasa kwa maana ya kwamba roho ya Nabii Ilyasa imemuingia yeye Hamza Issa na kwa hiyo yeye wamekuwa Nabii Ilyasa” alisema Sheikh

Aliongeza maelekezo na mafundisho ya uislamu yako wazi kuwa hakuna Mtume mwingine katika Uislamu baada ya Mtume Muhammad (S.A.W) na kwamba upatikanaji wa MTU ndani ya uislamu na kudai kuwa yeye ni Mtume ni kutaka kuamsha hisia Kali za waislamu nchini.

“Baraza la Ulamaa linapenda kuwafahamisha waislamu kwamba, yeyote atakayemfuata mpotoshaji huyu atakuwa ametoka ndani ya uislamu” alisema Sheikh Mataka.

Pia Baraza limetoa wito kwa Masheikh wa Mikoa, Wilaya na viongozi wa taasisi mbali mbali za Kiislam kutotoa fursa ya aina yoyote kwa huyo anayejiita Nabii ( Hamza Issa), ili kuzuia kuipotosha jamii.
Powered by Blogger.