Mkazi momoja wa Kitongoji cha Nyabuchinchibu kijiji cha Kerende kata ya
Kemambo Wilayani hapa mkoani Mara, Irabu Marwa (25) amefariki dunia baada ya
kuchomwa kisu na sehemeji yake kwenye bega la kushoto.
Marwa alifariki dunia muda mfupi baada kupata jeraha
hilo na kumsababishia kuvuja damu nyingi zilizomsababishia kufariki dunia
kabala ya kufika hospitalini.
Kamanda wa polisi mkoa wa Tarime na Rorya Kamishina
msaidizi Mwandamizi Henry Mwaibambe amethibitisha kutokea kwa tukio hilo
lililotokea julai 26 saa 2 usiku katika kijiji cha Kerende kata ya Kemambo
Wilayani hapa.
“Muuji ameoa mdogo wake marehemu, baada ya
kutekeleza tukio hilo alikimbia kusikojulikana lakini jeshi la polisi
linaendelea kuhakikisha kuwa anapatikana,”alisema SACP Mwaibambe.
Mwenyekiti wa kitongoji wa cha Nyabuchinchibu, Marc
Marwa alisema tukio hilo lilitokea julai 26 majira ya saa mbili usiku wakati
marehemu na shemeji yake walipokuwa wakinywa pombe.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kerende Mwita Magabe alisema kuwa alipata taarifa ya
kutokea kwa tukio hilo kwa njia ya simu majira ya saa mbili usiku na alipofika
karibu na eneo alithibitisha kuwa kweli Marwa alikuwa amefariki baada ya kuona
mwili wake.
“Ninakoishi hakuna mawasiliano ya simu lakini jioni
nikasema nisogee eneo la network ili nipate mawasiliano ndipo nilipata ujumbe
mfupi kuwa kuna tukio la mtu kuuawa na nikaanza safari ya kuja kwenye eneo la
tukio na kweli ndivyo ilivyokuwa,”alisema Magabe.
Hata hivyo Magabe alisema kuwa hilo ni tukio la pili
kutokea katika kijiji chake la watu kuchomana kisu na kufariki kwa muda wa kipindi cha mwezi mmoja na tayari yameishakaa
na kuweka mikakati ya jinsi ya kukomesha hali hiyo.
“Tumefanya mikutano miwili na kuweka faini ya sh,
200,000 kwa atakekutwa anatembea na panga au kisu, na kwa kushirikiana na wazee
wa mila, lakini hili limetokea tena, tunaomba jeshi la polisi wanapomkamata mtu
wa jinsi hii na kufikishwa mahakamani, mahakama isisubiri ushahidi,”alisema
Magabe.
Marwa Magabe ambaye ni mdogo wake Marehemu Irabu alisema kuwa marehemu alikuwa
na ugomvi wa siku nyingi na shemeji yake hivyo walikuwa wakitoleana maneno na
vitisho ya kufanyiana jambo lolote pale watakapokutana.
“Samwel Daudi (Aliyefanya mauaji) alitorosha mdogo
wetu hivyo Irabu akawa amekasirika kwa
kitendo cha kumtorosha na kutuharibia sifa ya familia na mpaka sasa anaishi na
mdogo wetu huyu, na marehemu ameacha mke na watoto watatu.
Changamoto sasa ni kwa shemeji jinsi ya kuwakuza
watoto hawa watatu maana mkubwa ana miaka mitano wa pili mitatu na wa mwisho
mmoja, kwetu hili ni pigo kubwa maana marehemu alikuwa tegemezi kwa
familia,”alisema Magabe.
|