Urusi Yaionya Marekani.....Yasema Itatungua Ndege Yoyote ya Muungano Unaoongozwa na Marekani


Urusi imeonya kuwa itashambulia ndege za muungano unaoongozwa na Marekani nchini Syria iwapo ndege hizo zitapaa katika maeneo ambayo jeshi lake linahudumu.

Hii ni baada ya ndege ya kivita ya Marekani kutungua ndege ya kivita ya serikali ya Syria.

Muungano huo unaoongozwa na Marekani ulisema ndege yake moja ilitungua ndege ya Syria aina ya Su-22 baada ya ndege hiyo kuwaangushia mabomu wapiganaji waasi wanaoungwa mkono na Marekani katika mkoa wa Raqqa, Jumapili.

Urusi, mshirika mkuu wa serikali ya Syria, imesema pia kwamba itakatiza mawasiliano yote na Marekani ambayo lengo lake huwa kuzuia ajali angani.

Syria imeshutumu shambulio hilo la Marekani na kusema litasababisha "matokeo mabaya sana".

"Ndege yoyote, ikiwa ni pamoja na ndege za kawaida na ndege zisizokuwa na rubani ambazo ni za muungano wa kimataifa unaohudumu magharibi mwa mto Euphrates, zitafuatiliwa na majeshi ya kukabiliana na ndege angani na ardhini na zitachukuliwa kama kitu kinachofaa kushambuliwa," wizara ya ulinzi ya Urusi imesema.

Urusi imekanusha madai kwamba Marekani ilikuwa imewasiliana na maafisa wa urusi kabla ya ndege hiyo aina ya Su-22 kutunguliwa.

Maafikiano kati ya Urusi na majeshi ya muungano unaoongozwa na Marekani ya kushirikiana kuzuia ajali angani na pia kuhakikisha usalama yalifika kikomo Jumatatu, wizara hiyo iliongeza.

Hii si mara ya kwanza mawasiliano kusitishwa kati ya pande hizo mbili.

Aprili, mawasiliano yalisitishwa baada ya Marekani kurusha makombora aina ya 59 Tomahawk katika kambi ya ndege za kijeshi ya Shayrat, nchini Syria.

Marekani ilishambulia baada ya Syria kudaiwa kutekeleza shambulio la kemikali katika maeneo yaliyoshikiliwa na waasi katika mkoa wa Idlib.

Lakini mataifa hayo mawili yalifufua mawasiliano yao mwezi uliopita.

Ndege hiyo ya kivita ya Syria aina ya Su-22 ilitunguliwa na F/A-18E Super Hornet karibu na mji wa Tabqa mkoa wa Raqqa Jumapili alasiri, wizara ya ulinzi ya Marekani imesema.

Inaaminika kwamba ndicho kisa cha kwanza kabisa cha ndege yenye rubani ya Marekani kutungua ndege nyingine ya kivita yenye rubani tangu vita vya Kosovo mwaka 1999.

Waasi wa Syrian Democratic Forces (SDF) wanaoungwa mkono na Marekani, wamekuwa wakihudumu eneo la Tabqa.

                                                  Credit: BBC
Powered by Blogger.