Taarifa Kwa Umma Kuhusu Wahitimu Wa Stashahada Katika Programu Mbalimbali Wanaokusudia Kuomba Kujiendeleza Katika Ngazi Ya Shahada Katika Vyuo Vya Elimu Ya Juu Kwa Mwaka Wa Masomo 2017/2018
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ni chombo kilichoanzishwa kwa Sheria ya Bunge, Sura 129, ili kusimamia na kuratibu utoaji wa mafunzo ya elimu ya ufundi nchini.
Jukumu kubwa la Baraza ni kuendeleza na kuinua ubora wa elimu na mafunzo ya ufundi nchini kwa kusimamia kikamilifu shughuli za usajili na ithibati, mitaala na upimaji ili tuzo zitolewazo na vyuo/taasisi ziwe na ubora unaokubalika kitaifa na kimataifa.
Kifungu cha 5 (1) (e) na (f) cha Sheria hii kinaipa mamlaka NACTE, kuanzisha tuzo mbalimbali zinazotolewa na kuhakikisha kuwa ubora wa elimu na mafunzo ya kada ya kati yatolewayo na taasisi mbalimbali yanazingatia ubora unaokusudiwa.
Aidha, Kifungu cha 11, kinalitaka Baraza kuhakikisha kuwa Tuzo zitolewazo na vyuo na taasisi zote zinazoendesha mafunzo ya kada ya kati zinatambuliwa na mamlaka husika. Katika muktadha huu, kila chuo/taasisi inayotoa elimu ya ufundi inatakiwa kuwasilisha Baraza matokeo ya mitihani kila mwisho wa semista.
Hivyo, kwa kuwa Udahili na uchaguzi wa wanafunzi kwa ajili ya masomo ya Shahada mbalimbali yanayotolewa na taasisi/vyuo vyote hapa nchini, utafanyika moja kwa moja vyuoni, Baraza linao wajibu wa kuziwezesha taasisi/vyuo hivyo kudahili wanafunzi wenye sifa stahiki.
Ili kulifanikisha hili, Baraza limeandaa mfumo ambao taasisi/chuo kitapata taarifa za muombaji mwenye sifa linganifu (muhitimu wa Stashahada) moja kwa moja.
Hivyo, wahitimu wote wa Stashahada yoyote wanaokusudia kuomba kujiendeleza katika ngazi ya Shahada wanatakiwa kuhakiki taarifa zao Baraza (NACTE) kabla ya kufanya maombi yao kwenye taasisi/vyuo wanavyotaka kwenda kusoma.
Uhakiki huo utafanywa kwa njia ya mtandao (online) kupitia Mfumo wa Uhakiki wa Tuzo (NACTE Award Verification System - NAVS) kwa kubofya hapa au kupiti tovuti ya NACTE (www.nacte.go.tz) kwa kubofya kitufe kilicho andikwa Award Verification.
Baada ya kuhakiki taarifa zake kuwa kamilifu na sahihi, mhakiki atapatiwa Namba ya Utambulisho (Award Verification Number - AVN) ambayo itaambatanishwa na maombi ya Udahili kwenye taasisi/chuo husika.
Utambulisho huo utatumiwa na taasisi/chuo kujiridhisha kwamba taarifa alizowasilisha muombaji wa Udahili ni sahihi na hivyo kuweza kudahiliwa na kisha kuchaguliwa kwa ajili ya masomo kulingana na mahitaji ya taasisi/chuo husika.
Aidha, Baraza linapenda pia kuwafahamisha wale wote walio na Stashahada walizopata nje ya nchi (Foreign Diploma Awards), nao waziwasilishe kupitia mfumo huu (NAVS) kwa ajili ya kuzifanyia ulinganifu na kuweka taarifa zao kwenye Kanzidata ya Baraza ili nao waweze kupata Namba ya Utambulisho. Maelezo ya namna ya kuziwasilisha tuzo za kufanyiwa ulinganifu yanapatika kwenye tovuti ya NACTE (www.nacte.go.tz).
Ili mwombaji Udahili apate Namba ya Utambulisho atalipa Shilingi Elfu Kumi (10,000/=) kwa njia ya mtandao (Online) kwa kufuata maelekezo yaliyopo kwenye Mfumo wa Uhakiki wa Tuzo - NAVS.
Kwa wale wanaotaka kufanya ulinganifu wa vyeti vyao, watatakiwa kulipa Shilingi Elfu Ishirini (20,000/=) kwa tuzo za ndani ambazo hazisimamiwi na baraza, na Shilingi Elfu Hamsini (50,000/=) kwa tuzo za nje ya nchi (foreign awards).
Baraza linapenda kuwafahamisha wahitimu wa Stashahada wanaotaka kujiendeleza katika ngazi ya Shahada kuwa wanaweza kufanya uhakiki huo kuanzia leo tarehe 28 Juni, 2017 hadi tarehe 20 Julai, 2017.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA KATIBU MTENDAJI
BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA UFUNDI (NACTE)
TAREHE: 28/06/2017