Rais Magufuli aizika rasmi BRN......Wafanyakazi wahamishiwa idara nyingine za Serikali


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 27 Juni, 2017 ameagana na wafanyakazi wa iliyokuwa Ofisi ya Rais, Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi (President’s Delivery Bureau – PDB) ambao wamehamishiwa katika ofisi na taasisi nyingine za Serikali kwa ajili ya kuendelea na utumishi wa umma.

Wafanyakazi hawa ndio walikuwa wakisimamia utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now – BRN).

Mhe. Rais Magufuli amekutana na wafanyakazi hao Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo amewashukuru kwa kazi nzuri waliyoifanya wakiwa PDB na amewataka kuendelea kulitumikia Taifa kwa juhudi na maarifa wakiwa katika ofisi nyingine walizopangiwa.

“Natambua kuwa nyie ni wafanyakazi wazuri wenye ujuzi na maarifa muhimu kwa ajili ya Taifa letu. Mmetoa mchango mkubwa mlipokuwa PDB nategemea mtaendelea hivyo na hata zaidi katika ofisi mbalimbali mlizopangiwa, mkachape kazi kwa kutanguliza maslahi ya Watanzania” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mhe. Angellah Kairuki, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dkt. Laurian Ndumbaro.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na timu ya wataalam wa masuala ya umeme na ujenzi wa miundombinu ya mabwawa ya maji kwa ajili ya kuzalisha umeme na kujadiliana nao kuhusu utekelezaji wa mradi mkubwa wa uzalishaji wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Power Project) ambao una uwezo wa kuzalisha Megawatts 2,100 za umeme.

Mhe. Rais Magufuli amekutana na wataalamu hao ikiwa ni utekelezaji wa nia yake ya kuhakikisha mradi huo unaanza kujengwa haraka iwezekanavyo na kuzalisha umeme mwingi utakaosaidia kuharakisha maendeleo hapa nchini, hususani ujenzi wa viwanda.

“Kesho Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe. Hailemariam Desalegn anawatuma wataalamu wake waliojenga mradi mkubwa wa bwawa la maji la kuzalisha umeme kule Ethiopia, wakiwa hapa mtakutana nao na mtabadilishana uzoefu, nataka na sisi tusichelewe, tuzalishe umeme utusaidie kwenye ujenzi wa viwanda” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
Powered by Blogger.