Nape Nnauye Awataka Wapinzani Waungane Na CCM Kumtetea Rais Magufuli Kwa Kupigania Raslimali Za Nchi
Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye amefunguka na kuwataka wabunge wa Chama Cha Mapinduzi na wale wa upinzani kuungana pamoja katika kupigania rasilimali za nchi katika vita ambayo imeanzishwa na Rais Magufuli.
Nape Nnauye amesema hayo bungeni na kuwataka watu wa CCM wasipuuze mawazo ambayo yanatolewa na watu wa upinzani na kusema wanapaswa kuyafanyia kazi ili mwisho wa siku nchi iweze kufaidika na rasilimali hizo na kuwafanya kuwa pamoja katika jambo hilo na si kunyoosheana vidole.
"Katika hili tunaweza kugawanyika katika mitazamo wapo wale wanaounga mkono asilimia mia moja, wapo wale wanaopinga kwa namna wanavyowaza wao sasa kelele zisiturudishe nyuma lazima tusonge mbele sababu vita hii ni takatifu.
"Lakini tusipuuze kwani katika kelele nyingi kunaweza kuwa na ushauri mzuri ndani yake, isifike mahali tukapuuza kabisa hii vita ni ya kwetu wote, nchii hii ikifaidika katika jambo hili ni faida kwetu wote bila kujali itikadi zetu za vyama, sasa tusitoboane macho, tusitupiane vijembe visivyokuwa na maana ni wakati wa kuileta nchi yetu pamoja twende pamoja vita hii tushinde, kwa hiyo wapinzani na CCM na watu wengine wote bila kujali itikadi zetu nadhani ni vizuri tukaungana katika hili" alisisitiza Nape Nnauye
Mbali na hilo Nape Nnauye alisema kuwa anachokifanya Rais Magufuli sasa anapita katika msingi ambao watangulizi wake waliuweka hivyo anadai viongozi hao wastaafu walifanya kazi kubwa kulinda rasilimali za nchi kwa uwezo wao, hivyo dhana ya kuona hawakuwa na jitihada za kulinda rasimali hizo si sawa.
"Hizi juhudi za kulinda rasilimali za nchi yetu hazijaanza awamu ya tano, zimeanza toka awamu ya kwanza ya mwalimu Nyerere kuna mambo alifanya kulinda rasilimali zetu hata kama kutakuwa na mapungufu, awamu ya pili ya mzee Mwinyi yapo mambo aliyafanya, awamu ya tatu ya mzee Mkapa yapo mambo aliyafanya, awamu ya nne ya Mhe. Kikwete yapo mambo ameyafanya mazuri tu, kwa hiyo hakuna namna tutapuuza juhudi zilizofanywa na watangulizi wa Mhe. Magufuli kwa sababu nao wana mchango hata kama leo itaonekana kulikuwepo na mapungufu lakini kwa nafasi zao walitimiza wajibu wao" alisema Nape Nnauye