NAMNA VIGOGO WA TFF WALIVYOHAHA PALE MAHAKAMANI KISUTU



Kufuatia Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kushikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), baadhi ya vigogo wa shirikisho hilo wamehaha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu iliyopo jijini Dar huku kazi zao zikisimama kwa muda.

Malinzi alishikiliwa na Takukuru tangu Juni 27 kwa ajili ya kuhojiwa na kufanyiwa uchunguzi huku akipandishwa kizimbani jana katika mahakama ya Kisutu.

Aidha, tangu bosi wao huyo ashikiliwe na Takukuru, maofisa mbalimbali wa TFF wameonekana kutotulia kutokana na kuhaha kutaka kujua undani wa suala lake ikiwa ni pamoja na kutaka kumtolea dhamana ambapo siku ya juzi hakuweza kufikishwa mahakamani na badala yake alifikishwa jana.

Miongoni mwa vigogo waliofika katika mahakama hiyo siku ya juzi ambao walishinda hapo tangu asubuhi ni pamoja na Mkurugenzi wa Vyama na Uanachama wa TFF, Eliud Mvela, Mshauri wa Ufundi wa Rais Malinzi, Pelegrinus Ruthayuga pamoja na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi ambao wote kwa pamoja walikuwa hawatulii kwa kufuatilia suala hilo Takukuru na Kisutu.


Aidha, kiongozi mwingine aliyeonekana akihaha ni pamoja na Mshauri wa Mambo Binafsi wa Malinzi, Juma Matandika ambaye alikuwa miongoni mwa wadau waliofika kulifuatilia tukio hilo kwa ukaribu zaidi pamoja na wadau mbalimbali wa michezo.


                  SOURCE: CHAMPIONI
Powered by Blogger.