MISWADA YA MADINI YATUA BUNGENI DODOMA
Ikiwa
ni siku kadhaa zimepita baada ya Rais John Magufuli kulitaka Bunge
lipitie upya sheria na mikataba ya madini, miswada mitatu inayohusu
madini tayari imesomwa bungeni kwa mara ya kwanza jana.
Aidha,
ili kutoa fursa ya wabunge kujadili miswada hiyo iliyowasilishwa
bungeni kwa hati ya dharura, vikao vya Bunge la Bajeti vilivyokuwa
vifikie tamati leo, vimesogezwa hadi Julai 5 mwaka huu ili kutoa fursa
kwa wabunge kupitia miswada hiyo.
Miswada
iliyosomwa kwa mara ya kwanza bungeni hapo ni Muswada wa Sheria ya
Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili
za Nchi wa Mwaka 2017.
Muswada
huu unapendekeza kuweka utaratibu ambapo wananchi kupitia chombo chao
cha uwakilishi ambacho ni Bunge, kitapitia na kujadili makubaliano na
mikataba yote inayohusu rasilimali za nchi, ambayo imefungamana na
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kujiridhisha na masharti.
Muswada mwingine ni Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya nchi Kuhusu Umiliki
wa Maliasili wa mwaka 2017.
Muswada
huu unakusudia kuweka masharti yatakayohakikisha kwamba hatua yoyote
inayochukuliwa kuhusu uwekezaji wa rasilimali za taifa, inatambua na
kuzingatia haki ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama taifa huru lenye
mamlaka ya kusimamia na kutumia rasilimali zake kwa maslahi ya taifa.
Muswada mwingine ni Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria
Mbalimbali wa mwaka 2017.
Wakati
anapokea ripoti ya pili ya Kamati Maalumu ya Uchumi na Sheria kuhusu
Taarifa ya Makinikia, Rais Magufuli aliliomba Bunge kupitia upya sheria
na mikataba yote ya madini na gesi ili kuiepusha nchi kuingia katika
mikataba mibovu.
“Kamati
ya uongozi ilikaa jana (juzi) kubadilisha ratiba ambapo sasa mkutano
huo wa Bunge la bajeti utaahirishwa Julai 5 mwaka huu, badala ya Juni 30
kama ilivyokuwa imepangwa awali, miswada mitatu mipya ya sheria
iliyosomwa kwa mara ya kwanza, itapelekwa katika kamati za Bunge,” alisema Spika Job Ndugai, ili kutoa nafasi kwa wabunge kujadili miswada hiyo,.
Bunge limebadili ratiba kwa Bunge kuendelea na shughuli zake hadi Julai 5 mwaka huu, ambapo bunge hilo litaahirishwa.
Alisema
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa mwaka 2017 kwa
kuangalia upungufu uliojitokeza itafanyiwa kazi na Kamati ya Kudumu ya
Katiba na Sheria inayoongozwa na Mohammed Mchengerwa.
Ndugai
alisema pia Bunge limeunda kamati maalumu itakayoundwa na wajumbe wa
kamati nne za Nishati na Madini, Kamati ya Ardhi, Kamati ya sheria
Ndogondogo na Kamati ya Katiba na Sheria, itakayoongozwa na Mwenyekiti
wa Kamati ya Nishati na Madini, Dotto Biseko ambayo itapitia miswada
miwili ya Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika
Mikataba ya Maliasili za Nchi wa mwaka 2017.
Pia kamati hiyo itafanyia kazi Muswada wa Sheria ya Mamalaka ya nchi kuhusu Umiliki wa Maliasili wa mwaka 2017.
“Kamati
hizo zitafanya kazi kuanzia leo (jana) kwa kukutana na wadau mbalimbali
na kisha taarifa itawasilishwa bungeni Jumanne, kabla ya bunge
kuahirishwa Jumatano (Julai 5 mwaka huu),”
Baada
ya kuwasilishwa kwa miswada hiyo, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika
aliomba mwongozo wa Spika, ambapo aliliomba bunge kuondoa hati ya
dharura ya kujadili miswada hiyo.
“Muda
mfupi uliopita tumekabidhiwa ratiba ya bunge, serikali inaleta miswada
mitatu kwa hati ya dharura, mwaka 1997 mikataba ya madini ilipitishwa
haraka haraka, mikataba ya ngesi hivyo hivyo,
“Kazi
ya bunge ni kutunga sheria, sisi ndio wawakilishi wa wananchi, kwa
umuhimu wake na maslahi kwa wananchi, sisi wawakilishi tulitakiwa
kukutana na wananchi, hivyo ni bora ikasomwa leo kwa mara ya kwanza na
hati ya dharura ikaondolewa na kuletwa bunge lijalo.
“Kwa
maelezo uliyotoa wadau wataitwa kwa short notice wafike Dodoma
kujadili, sisi wabunge vile vile, miswada mitatu inaletwa tuichambue.
Huu ni mtego kwa kutufanya tushindwe kuishauri serikali kwa kazi yetu ya
kibunge”.
Akitoa
majibu ya serikali kuhusu muongozo huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulamavu, Jenista
Mhagama alisema masharti ya kutunga sheria na masharti ya jumla,
yamewekwa katika fasihi ya nane ya Kanuni za Bunge, masharti yameongezwa
na kanuni ya 80 na kanuni nyingine.
“
Muswada ambayo imeletwa imekuja kwa hati ya dharura, ili bunge liridhie
kama miswada hii inastahili kujadiliwa na bunge ama la, kanuni 80(4)
inasema muswada wowote wa dharura hautaingizwa katika shughuli za Bunge
bila kuwa na hati iliyowekwa sahihi na rais kuthibitisha kwamba muswada
huo ni wa dharura.
“Sisi
kama serikali tumeshatimiza masharti yote, tumeshakamilisha hatua zote
za kufikishwa muswada huo kwa hati ya dharura. Wanaoweza kulishauri
Bunge baada ya kuona uzito wa kazi iliyolewa na serikali ni kamati
husika itakayopewa kazi ya kujadili miswada hiyo,” alisema.
Alisema
sio busara kwa wabunge kabla hawajaona yaliyomo katika miswada husika,
kujenga hoja ya kuikataa ndani ya bunge, mana kinachofanyika ni kwa
maslahi mapata ya taifa.
Akijibu
mwongozo huo, Spika Job Ndugai alisema kwa niaba ya wabunge alipokea
hati ya dharura huku akiwataka wabunge kulifanyia kazi jambo hilo.
“Tulijadiliana
na kamati ya uongozi yenye uwakilishi wa tukakubaliana suala hili
lisonge mbele. Wakati Rais (Magufuli) akipokea ripoti ya pili ya
mainikia, kwa niaba yenu nilikubali kama kuna mambo yenye maslahi kwa
nchi tutayafanyia kazi, mambo yameletwa katika kamati husika, kamati
itajadili kama muswada inastahili kuingia bungeni ama la hoja nitatokea
huko.
Aliongeza, “kwa
muda mrefu tulikuwa tunataka Bunge kuwa na nafasi fulani katika masuala
yanayohusu maadini na gesi, liwe na nafasi fulani ili kuzuia nchi
kuingia katika mikataba mibovu.
“Miswada hii kama mtanzania yeyote mwenye kuhitaji ataipata katika tovuti,”alisema Ndugai.